Subscribe:

Sample text

Sample Text

About Us



HABARI BINAFSI
Kwa majina ni: LUKA ROKI CHAMAYOMBE.  Jina hili la tatu siyo jina la ukoo; wala si jina la babu yangu bali ni jina ambalo baba yangu alijipa mwenyewe na mimi naliendeleza tu. Jina la babu ni “SESIYAMOTO” maana “CHECHEYAMOTO” Majina yangu ya uzaliwa/ukoo ni Kusinile, Maghali au Mihengo.  
Nimezaliwa tarehe 8/4/1937 katika kitongoji cha Misegese, Tarafa ya  Mlali, Wilaya ya Morogoro Vijijini, wakati huo (kwa sasa Wilaya ya Mvomero) Mkoani Morogoro. Nimebatizwa tarehe 26/5/1937 Parokia ya Mgeta, Jimbo la Morogoro.
Kimasomo, kwa muda wa miaka kadhaa hadi 1949 nilisoma Bush School ya Peko. Miaka 1950-1952 niliendelea na elimu ya msingi hadi darasa la IV katika shule ya msingi Kigurunyembe. Miaka 1953-1959 niliendelea na masomo Bagamoyo Seminari ndogo ya Mt. Petro. Miaka 1960-1961 niliendelea na masomso katika Seminari ndogo ya Mt. Maria Nyegezi Mwanza, ambako nilifannyia na kufuzu mitihani ya “Cambridge” ya Darasa la XII.  Miaka 1961-1962 nikaendelea na masomo katika Seminari Kubwa ya Mt. Thomas Kilakala Morogoro.  Kutokana na kufungwa kwa Seminari Kubwa ya Mt. Thomas mwaka 1963 nikahamia Seminari Kubwa ya Kipalapala Mkoani Tabora ambako mwishoni mwa mwaka 1966 nikafanikiwa kuacha kusomea upadre kwa kukubali kwenda kufundisha Seminari Ndogo ya Mt. Pius Makoko Wilayani Musoma mkoa wa Mara kwa Mwaka mmoja 1967.
Mwaka 1968 nikaajiriwa Serikalini katika Wizara ya Maendeleo Vijijini. Miaka 1976-1979 nilipata likizo ya miaka 3 ambayo nilitumia kusomea “Advanced Diploma in Business Administration” IDM Mzumbe Morogoro. Baada ya Masomo hayo nikahamishiwa Wizara ya Biashara hadi nilipostaafu kama Afisa Biashara Mwandamizi III mnamo April 1992.  
Mwaka 1995 nikajiunga na Karismatiki Katoliki Mzumbe, Morogoro. Tangu hapo nikawa miongoni mwa wapeleka Injili Maparokiani Jimboni Morogoro; na nje ya Jimbo la Morogoro kama vile Iringa, Ilongero-Singida, Kigonsela-Mbinga, Ngaramtoni mkoani Arusha na Ngong’ nchini Kenya.
Lakini kadiri nilivyoukulia ukweli wa Mungu ndivyo wengi walivyoshindwa kunielewa kabisa. Hata ikafikia wakati nikanyimwa fursa ya kuhubiri. Kwa ufahamu niliokuwa nimeufikia katika kuukulia ukweli wa Mungu, nikayapuuza hayo yote. Nikaamua kusonga mbele na wale tu wasiopenda utukufu wa mwanadamu kuliko utukufu wa Mungu (Yn.5:41,44; 12:43). Nami, katika uwanja wa kuukulia ukweli wa Mungu, nikawa namuhesabu mtu yeyote anayependa utukufu wa wanadamu kuliko wa Mungu kweli, kuwa ni fira. Hivyo, hiyo imekuwa ndiyo hali halisi katika kuukulia ukweli wa Mungu wa pekee wa kweli.
Mungu hutaka watu wote waokolewe na kupata kujua iliyo kweli (1Tim.2:4), maana watu wake hupotea kwa sababu ya kutojua maandiko wala uweza wa Mungu (Mt 22:29). Hatimaye atuambia, “mkiyajua hayo, heri ninyi mkiyatenda”. (Yn 13:17) na kinyume cha “Heri” ni “Ole”.  Hivyo, kwa sababu zilizotolewa katika Ebr.6:4-6 na 2 Pet.2:20-22, mimi sitarudi nyuma.  Kwa utendaji wa Mungu Roho aliye katika Nafsi Tatu: Kweli, Neno na Roho wa kweli, hakuna neno lolote lisilowezekana; bali kuna kushinda na zaidi ya kushinda kwa Yeye atupendaye upeo (Yn.13:1) kwa upendo wa milele (Yer.31:3) na ambaye haachi kujishughulisha kwa mambo  yetu (1Pet. 5:7); maaana Yeye aweza kufanya mambo ya ajabu mno, kuliko yote tuombayo au tuwazayo kwa kadiri ya nguvu itendayo kazi ndani yetu milele yote (Efe.3:20).
Kwa utendaji wa Roho Mtakatifu nafsini mwangu, ninaamini kikwelikweli 100% kwamba nahesabiwa kuwa mwenye haki wa Mungu kutokana na neema au zawadi ya  Damu ya Yesu  Kristo Neno la Mungu. Naamini kwamba utakaso huo umefuatiwa mara moja na kunyweshwa Roho Mtakatifu na kumvaa Kristo Neno la Mungu kuwa Roho moja Naye; Kristo yu ndani yangu nami nimo ndani yake. Na hivyo, Mungu Roho aliye katika Nafsi Tatu yumo ndani yangu, nami ndani yake.  Hivyo, ufalme wa mbinguni umo ndani yangu kwa sababu Mungu Roho aliye Nafsi Tatu Yumo ndani yangu hapa duniani, nami nimo ndani yake katika ulimwengu wake wa Roho, Mbinguni.  Haniachi yatima. Yuko nami kotekote wakati wote. Hivyo niko mzima, salama na mshindi katika yote wakati wote. Ni raia ya ufalme wa Mungu pekee wa kweli (Phil. 3:20), kwa huyo Roho wa kweli niliyenyweshwa (1Kori 12:13: 1Yoh 3:24).

0 comments:

Post a Comment