Tunasoma katika Rum.3:23-26 kwamba wote wamefanya dhambi na
kupungukiwa na utukufu wa Mungu; kwamba wanahesabiwa haki bure kwa njia
ya ukombozi ulio katika Kristo Yesu; ambaye Mungu amekwisha kumweka awe
upatanisho kwa njia ya imani katika DAMU yake, ili aoneshe haki yake
kwa sababu ya kuziachilia katika ustahimili wa Mungu dhambi zote
zilizotangulia kufanywa; apate kuonesha haki yake wakati huu; ili awe
mwenye haki na mwenye kumhesabia haki yeye amwaminiye Yesu.
Mshahara wa dhambi ni mauti (Rum.6:23); Mungu wa pekee wa kweli, kwa
wema na upendo wake mkuu anaowapenda watu wake upeo (Yn.13:1) kwa
upendo wa milele (Yer.31:3), na kwa uvumilivu wake usiopimika, akaazimia
kufanya mpango wa kumrudisha mtu wake na kumfufua au kumhuisha kwa
upya.
Ili hili lipate kutimilika, sharti kile kifarakanishi
kilichomfanya aachane na mtu wake, dhambi, kiondolewe kwanza, kisiwepo
“tena” ndani ya mpendwa wake.
Lakini dhambi ni mlima mkubwa mno
kuweza kushughulikiwa na mtu au kiumbe chochote duniani, hata mbinguni.
Zaidi ya hilo, ni kwamba katika hali ya dhambi, kiuhalisia, utu wa
ndani, utu halisi, yaani nafsi imekufa, ni marehemu, kutokana na ukweli
kwamba mshahara wa dhambi ni mauti. (Rum.6:23). Na maiti haiwezi
kufanya lolote kujikwamua katika umauti wake, wala kumsaidia mwingine.
Ndipo Mungu mwenyewe, katika kujikombolea mtu wake, akaamua kuwa ndani
ya Mungu Mwana, Neno, kuwapatanisha wanadamu na Nafsi yake mwenyewe
asiwahesabie makosa yao (2 Kor.5:19); bali kwamba wawe wenye haki
(watakatifu) wake katika Kristo Mwanawe wa pekee (2Kor.5:21).
Kwamba kwa upatanisho ambao huhitimishwa kwa njia ya imani katika nguvu
za Damu ya Yesu aliyefanywa kuwa dhambi, Mungu katika ustahimili wake,
huziachilia, yaani huzifuta dhambi zilizotangulia kufanywa (Rum.3:25),
na wala hazikumbuki tena kabisa (Ebr.10:17). Na ndipo Mungu kwa amani
tele humnywesha (Kor.12:13) na kumvalisha utimilifu wote wa Mungu
(Gal.3:27) ili mtu awe mwana wa Mungu (Gal.3:26).
Hapo ndipo mtu
anapokuwa ametimilika kwa utimilifu wote wa Mungu (Effe.3:19).katika
Kristo Yesu aliye kichwa cha kila enzi na mamlaka (Kol.2:9-10). Hapo
mambo huwa kama Mungu alivyo, ndivyo mtu naye anavyokuwa hapa duniani
(1Yon.4:17).
KUPATANISHWA NA MUNGU YUPI? KUHUSU NINI?
Tatizo
linalotukabili binadamu ambalo ibilisi amewafunga na kuwagharagaza
binadamu ni utumwa wa dhambi (Yn.8:34). Na ndilo hilo Yesu ametumwa
kuja kulishughulikia atutoe tuwe huru (Mt.1:20-21).
Mungu
mwenyewe, katika Umoja wake wa Utatu Mtakatifu, amelishughulikia swala
la upatanisho kiutimilifu. Ona alivyolianza katika ile Sala yake Kuu
kama tunavyosoma katika Yn.17. Kisha tuone Mungu anavyoitenda katika
Nyaraka za Mitume. Hebu soma Rum.8:26-27, 34; 2Kor.5:19; Ebr.7:25;
1Yn.2:1-2.
Nje ya hapo ni uzushi mtupu kama tunavyoambiwa katika Kol.2:23, na matunda yake kama tunavyodhihirishiwa katika Gal.5:19-21.
Mt.12:33-35 hutuagiza: “Ufanyeni mti kuwa mzuri na matunda yake kuwa
mazuri; au ufanyeni mti kuwa mbaya na matunda yake kuwa mabaya. Maana
kwa matunda yake mti hutambulikana. Enyi watoto wa nyoka mwawezaje
kunena mema mkiwa wabaya? Maana kinywa cha mtu huyanena yaujazayo moyo
wake. Mtu mwema katika akiba njema, hutoa yaliyo mema; na mtu mbaya
katika akiba mbaya hutoa mabaya”.
Na katika Gal.5:16-18 twasoma,
“Basi nasema, Nendeni kwa Roho, wala hamtazitimiza kamwe tamaa za mwili.
Kwa sababu mwili hutamani kushindana na Roho, na Roho kushindana na
mwili; kwa maana hizi zimepingana, hata hamwezi kufanya mnayotaka.
Lakini mkiongozwa na Roho hampo chini ya sheria”.
Sasa sisi, kwenye dini zetu, hata amri za Mungu hazitutoshi. Tunajiongezea na lukuki lwa sheria nyinginezo nyingi tu.
Swala lililopo ni, Je, tutaanza lini kuwa waaminifu kwa Injili kama
tulivyoagizwa na Papa Yohani Paulo II? Je, tutaacha lini kujikabidhisha
kwa mungu wa dunia hii ambaye hupofusha fikira zao wasioamini
isiwazukie nuru ya Injili ya utukufu wake Kristo aliye sura yake Mungu
(2 Kor.4:3-4); na ambaye huwapelekesha watu wa Mungu kwa makristo
wengine na maroho, mengine mengine tu? Na hata pengine kujiinua katika
Jina la Mzazi wetu Bikira Maria?
Tutaachana lini na ile roho ya
upotevu ambayo hupofusha macho na kufanya mioyo mizito watu wasije
wakaona kwa macho yao na kufahamu kwa mioyo yao wakamongokea Kristo wa
kweli akawaponya (Yn.12:40)?.
Je watu wa Mungu waendelee
kuangamizwa hivi mpaka lini? Mpaka lini kazi ya Mwana wa Mungu
aliyoifanya pale Msalabani itaendelea kupuuziwa? Je, mpaka lini
tutaendelea kumdhihaki Mungu kwa kusali sala ya “Baba yetu…..”
tukimwambia “Ufalme wako ufike, utakalo lifanyike….” pindi tunakuwa
vizingiti au vikwazo kwa Ufalme wa Mungu na mapenzi ya Mungu ambaye
hutaka watu wote waokolewe na kupata kujua yaliyo kweli? Je, kusali
sala ile kuko mbali na unafiki:? Unafiki huu utaisha lini hata
tumkaribie Mungu wetu wenye moyo wa kweli kwa utimilifu wa imani
(Ebr.10:22).
Tumemdhihaki Mungu wetu wa pekee wa kweli Umoja wa
Nafsi Tatu Kweli na Neno na Roho wa Kweli kiasi cha kutosha, kwa
kulipuuza lile agizo la kwenda kwa Roho (Gal.5:16) na la kuufanya mti
kuwa mzuri. Sasa tuseme BASI!!! Twendeni kwa Roho na kuufanya mti kuwa
mzuri, badala ya kung’ang’ana na yaliyopitwa na wakati.
TWENDE KWA ROHO
Tumeona kwamba Gal.5:16 yatutaka twende kwa Roho ndipo hatutazitimiza
kamwe tamaa za mwili. Na Kol.2:8 yatuangalisha tusije tukafanywa mateka
kwa elimu ya bure na madanganyo matupu; kwa jinsi ya mapokeo ya
wanadamu, kwa jinsi ya mafundisho ya awali ya ulimwengu, wala si kwa
jinsi ya Kristo.
Injili yatutaka kwenda kwa jinsi ya Kristo.
Jinsi ya Kristo ni ipi?, Bwana Yesu ametupatia sharti lake la mtu kuwa
mwanafunzi wake ni kukaa katika Neno lake (Yn.8:31-36).
Injili
inatuhakikishia kwamba uhakika wa usalama dhidi ya dhambi uko katika
Neno lake. Anawaambia wafuasi wake, “Ninyi mmekuwa safi kwa sababu ya
lile neno nililowaambia (Yn.15:3).
Katika ile Sala yake kuu
amwambia Baba, Neno lako nimewapa, ulimwengu umewachukia kwa sababu wao
si wa ulimwengu kama mimi nisivyo wa ulimwengu (Yn.17:14).
Tena
amwambia Baba, “Uwatakase kwa ile Kweli; Neno lako ndiyo kweli. Mimi
najiweka wakfu mwenyewe ili na hao watakaswe katika kweli (Yn.17:, 19).
Efe.5:25-27 yatuambia kwamba Kristo Yesu ametoa Nafsi yake makusudi
alitakase na kulisafisha Kanisa lake kwa maji safi katika Neno.
N.B.
Tatizo kubwa linalojitokeza ni matumizi ya karatasi. Katika ujumla
wake, nafasi zilizo wazi ni sawa, kama siyo zaidi na nafasi zilizotuika.
Ebr.10:19-23 yatuhakikishia kwamba Kuhani Mkuu ametuosha miili kwa maji
safi yaliyomo katika Damu yake ambaye ni Roho Mtakatifu (Yn.4:10, 14;
7:37-39) ambaye ni Neno la Mungu (Yn.6:63).
Utimilifu wote uko
katika Kristo Yesu aliyekuja katika Maji na katika Damu (1Yn.5:6). Huko
ni kwenda kwa jinsi ya Kristo (Kol.2:8); na ndiko kwenda kwa Roho
(Gal.5:16); na ndiko kwenda kwa Hekima iliyoshuka kutoka mbinguni
(Yak.3:15; 1Kor.1:24).
Nje ya hapo ni kwenda kwa hekima ya dunia
na ya shetani. Na kama tulivyoambiwa katika Gal.5:17, nafsi ya mtu
haiwezi kufanya inavyotaka, hekima ya dunia, hekima ya kwenda
kimwilimwili ni hekima ya Mungu wa dunia hii, mpofushaji wa fikira, roho
ya upotevu ifanyayo watu wapotee njia ya kumfikia Baba katika ulimwengu
wake wa Roho (Efe.2:6).
UMUHIMU WA KUZINGATIA 100% ANGALISHO LA KOL.2:8-10
Angalisho la Kol.2:8-10 lapelekea kutufikisha kwenye ukweli kwamba
tatizo la utumwa wa dhambi haliwezi kutatuliwa kwa taratibu za kidini za
wakati wowote ule.
Taratibu za kidini kama vile Sabato, Sikukuu,
Kuungama (1Mfal.8:46-50; Nehemia 1:4-11), kuombea wafu (2Mak.12:38-46)
n.k. zilikwisha kuwako duniani. Lakini zote hazikufaa kitu katika
kulikabili tatizo la utumwa wa dhambi.
Utatuzi wa tatizo la dhambi uko katika kuufanya mti uwe mzuri ili matunda yake yapate kuwa mazuri (Mt.12:33-35).
Yesu amekuja kumfanya mtu azaliwe katika umungu kwa upya (Yn3:3, 5).
Amekuja kumshirikisha umungu kwa upya, ili mtu aweze kujilinda hata
asiguswe na yule mwovu (Yn.5:18). Ili hili litimilike sharti kwenda kwa
jinsi ya Kristo (Kol.2:8). Na jinsi ya Kristo ni ile iliyoelekezwa
katika Yn.8:31-32, 36 na Gal.5:16.
Kwa njia hiyo mtu hupata
kufikia utimilifu wote wa Mungu (Efe.3:19 na kuwa kama Mungu mwenyewe
alivyo (1Yn.4:17). Hapo mtu huwa ana mti mzuri, na matunda yake huwa
mazuri. Hapo mtu hawezi kutenda dhambi, kwa sababu amezaliwa kutokana
na Mungu kwa huyo Roho wa kweli aliyemnyweshw (1Kor.12:13) kumfundisha
yote kumkumbusha yote (Yn.14:26), kumwongoza katika kweli yote
(Yn.16:13), kumfundisha yote (1Kor.2:10) na kumwombea kama Baba
apendavyo (Rum.8:26-27).
Kwa utendaji huo wa Roho wa kweli,
dhambi haitafurukuta tena katika mtu aiaminiye kazi ya Mungu pekee wa
kweli katika Mwanawe Neno ambaye ni kweli (Yn.17:17).
Basi ndugu
yangu! Mungu wa pekee wa kweli, Baba wa Bwana wetu Kristo Yesu na Baba
yetu naakubariki wewe pamoja na ndugu wote kwa Baraka zote za rohoni
katika ulimwengu wa Roho ndani yake Kristo Yesu, sasa na hata milele.
Amina!!!
LUKA ROKI MAGHALI CHAMAYOMBE
0714 118 428
0787 765 759
0753 298 707
chamayombe37@gmail.com
Subscribe to:
Post Comments (Atom)



0 comments:
Post a Comment