Kwa kadiri ya Bibilia Takatifu, Mungu wa pekee wa Kweli ni Roho
(Yn.4:24) aliye katika Umoja wa Nafsi Tatu ambazo ni Baba, na Neno na
Roho Mtakatifu (1Yoh.5:8, toleo la Kimataifa au 1 Yoh.5:7 toleo la Agano
Jipya tu).
Kwa kadiri ya Yn.8:26, Baba aliyemtuma Mwana ni “KWELI”,
na Nafsi “NENO” ndiye Mwana kwa Jina lake halisi katika kweli
(Ufu.19:12-13). Kwa Nuru hiyo, Mungu wa pekee wa Kweli ni Roho aliye
katika Umoja wa Nafsi Tatu ambazo ni Nafsi Kweli, na Nafsi Neno na Nafsi
Roho Mtakatifu. Nafsi hizi Tatu ni Mungu mmoja, Roho asiyegawanyika.
JE? MUNGU HUYU WA PEKEE WA KWELI, ROHO ALIYE KATIKA UMOJA WA UTATU WAKE MTAKATIFU ANAKAA WAPI?
Katika hali yake ya kutoweza kugawanyika ni kwamba kila Nafsi miongoni
mwao hukaa katika kila Nafsi miongoni mwao. Kwamba kila Nafsi Miongoni
mwao, ni Maskani au Makao ya kila Nafsi miongoni mwao.
Hivyo,
Maskani ya Umoja wa Nafsi Tatu Takatifu ni Umoja wa hizo Nafsi Tatu
zenyewe. Hivyo, huo Umoja wa Nafsi Tatu wenyewe ndiyo mbinguni hasa
anakokaa Mungu Roho aliye katika Nafsi Tatu Takatifu: Kweli, ambaye ni
Baba, na Neno, ambaye ni Mwana, na Roho Mtakatifu.
JE? UFALME WA MUNGU ROHO ALIYE KATIKA UMOJA WA NAFSI TATU NI UPI?
Ufalme wa Mungu Roho aliye Umoja wa Nafsi Tatu Takatifu ni huo Umoja wa Nafsi hizo Tatu ambao muundo wake ni kama ifuatavyo:-
(1) Nafsi Kweli ambaye ni Baba ndiye Mfalme.
(2) Nafsi “NENO” ambaye ni Mwana ndiye Waziri Mkuu peke yake anayesimamia yote.
(3) Na Nafsi “ROHO” Mtakatifu ndiye Katibu Mtendaji anayetekeleza yote.
Hapo Ufalme wa Mungu huyu umetimilika 100%.
Baada ya kumfahamu Mungu wa pekee wa Kweli, Maskani yake na Ufalme
wake, hebu tuone maombezi ya Yesu kwa ajili yetu, Mwana amwambia Baba,
“Baba, hao ulionipa nataka wawe pamoja nami popote nilipo, wapate na
kuutazama utukufu wangu ulionipa;….” (Yn.17:24).
Na kabla ya kusema
hilo alimwambia Baba “Wote wawe na Umoja; kama wewe, Baba, ulivyo ndani
yangu, nami ndani, yako; hao nao wawe ndani yetu; ile Ulimwengu upate
kusadiki ya kwamba wewe ndiwe uliyenituma. Nami utukufu ule ulionipa
nimewapa wao; ili wawe na umoja kama sisi tulivyo Umoja. Mimi ndani yao,
nawe ndani yangu, ili wawe wamekamilika katika umoja; ili ulimwengu
ujue ya kuwa ndiwe uliyenituma, ukawapenda wao kama ulivyonipenda mimi
(Yn.17:21-23).
Katika maombi haya. Nii wazi kabisa kwamba Kristo
Neno la Mungu anataka watu wake wakamilishwe kwa kuingizwa na
kujumuishwa katika ule Umoja wa Nafsi Tatu Takatifu, Kweli na Neno na
Roho Mtakatifu.
Katika Ebr.10:14 imeandikwa “Maana kwa toleo moja
amewakamilisha hata milele hao wanaotakaswa. Hao wanaotakaswa,
wanatakaswaje? Wanaotakaswa wanatakaswa kwa ile dhabihu, yaani Damu ya
Yesu iliyotolewa mara moja tu na idumuyo hata milele (Ebr.10:10, 12).
Hao wanakamilishwaje? Hao wanakamilishwa kwa kubatizwa katika Roho
Mtakatifu kuwa Mwili wa Yesu kwa kunyweshwa Roho Mtakatifu (1
Kor.12:13). Na kwa Ubatizo huo wahusika huwa wamamvaa Kristo
(Gal.3:27)). Katika ujumla wake, wahusika huwa wananyweshwa na
kuvalishwa utimilifu wote wa Mungu (Efe.3:19; Kol.2:9-10). Hapo
wahusika huwa wamekamilishwa katika Ukamilifu wa Mungu pekee wa kweli,
Roho aliye katika Umoja wa Nafsi Tatu: Kweli na Neno, na Roho
Mtakatifu.
Maana, kama anavyosema katika 1Yoh.4:13 “katika hili
tunafahamu ya kuwa tunakaa ndani yake, naye ndani yetu, kwa kuwa
ametushirikisha Rono wake”. Na katika aya ya 17 tunasoma “Katika hili,
pendo limekamilika kwetu, ili tuwe na ujasiri katika siku ya hukumu, kwa
kuwa, KAMA YEYE ALIVYO, ndivyo tulivyo na sisi ulimwenguni humu”.
Hapo ombi la Kristo Neno la Mungu, Yn.17:21-24, limetekelezwa 100%.
Watu wake tumezaliwa katika Mungu Roho aliye katika Umoja wa Nafsi zile
Tatu. Hapo sisi sote tumekuwa wazaliwa wa Mungu Roho aliye katika Umoja
wa Nafsi Tatu Takatifu. Hapo sisi sote tumo ndani ya Umungu Roho ulio
katika Nafsi Tatu za Mungu wa pekee wa kweli. Hapo sisi sote, hapa hapa
duniani tulipo, tumo ndani ya Ufalme wa Mungu wa pekee wa kweli. Hapo
sisi sote tumo mbinguni, Umoja wa Nafsi Tatu Takatifu, hapa duniani
tulipo (Yn.17:14-15).
Ndipo tunapoambiwa, “Kila akaaye ndani yake
hatendi dhambi. Kila atendaye dhambi hakumwona Yeye, wala hakumtambua.
Kila mtu aliyezaliwa na Mungu hatendi dhambi, kwa sababu uzao wake
wakaa ndani yake; wala hawezi kutenda dhambi kwa sababu amezaliwa
kutokana na Mungu (1Yoh.3:6, 9).
Na katika 1Yoh.5:18 twasoma,
“Twajua ya kuwa kila mtu aliyezaliwa na Mungu hatendi dhambi; bali yeye
aliyezaliwa na Mungu hujilinda, wala Yule mwovu hamgusi”. Katika hili,
ibilisi yuko kazini kukupofusha wewe rafiki na ndugu yangu, kukupofusha
na kufanya nafsi yako iwe nzito kuufahamu ukweli huu eti wewe
usimwongokee Mungu wa pekee wa kweli akuponye (Yn.12:40 na 2Kor.4:3-4).
Kazi hii shetani ameifanya na anaifanya. Na pengine wewe mwenzangu
bado unaendelea kuwa mhanga (victim) wake ibilisi. Kwa uzima wa kweli
na kwa usalama wako, rafiki, sasa hiyo iwe basi. Wakati uliokubalika na
wa kusaidiwa na Roho Msaidizi ni sasa (2Kor.6:2).
Mungu ameendelea
kukuhifadhi mpaka sasa, kwa sababu hapendi mtu yeyote, ikiwa pamoja na
wewe hapo, apotee. Kamwe, usiendelee kumkanyaga Mwana wa Mungu, na
kuihesabu Damu ya Kristo Neno la Mungu uliyotakaswa kwayo kuwa ni kitu
ovyo, na kumfanyia jeuri Roho wa neema. Hakikisha unauingia Umoja wa
Nafsi Tatu, sasa hivi. Hakikisha unauingia Umoja wa Nafsi Tatu, sasa
hivi. Hakikisha unaingia mbinguni hivi sasa. Kamwe usingoje maji
yamwagike ndipo eti wengine wajitahidi kukuzolea. Hayazoleki. Mbinguni
unaingia wewe mwenyewe kwa kusaidiwa na Roho wa Kweli sasa hivi. Ndiyo
maana ilibidi Kristo Neno la Mungu azaliwe katika Ubinadamu na kuja
kwetu. Vinginevyo, angetungojea huko huko. Tuache kukubaliana na
shetani anayewafanya watu wamwone Mungu wa Kweli ni mpumbavu katika
mpango wake.
Rafiki na ndugu yangu katika Kristo Neno la Mungu,
uendelee kubarikiwa kwa Baraka zote za Kiroho katika ulimwengu wa Roho
ndani yake Kristo Neno la Mungu (Efe.1:3)
LUKA ROKI MAGHALI CHAMAYOMBE
0787 765 759
0714 118 428
0753 298 707
Chamayombe37@gmail.com
Wednesday, 4 October 2017
Subscribe to:
Post Comments (Atom)



0 comments:
Post a Comment