Kati ya yale maeneo nyeti matano ambayo yamebainishwa katika kifungu
cha 79 cha ile Barua “Ut Unum Sint”, tumekwisha kulipitia lile neneo
linalomhusu Mama yetu Bikira Maria, na lile linahusu mahusiano kati ya
Maandiko Matakatifu na Mapokeo Matakatifu. Na katika hali hiyo, sasa
tumebakiwa na maeneo matatu ambayo ni:-
(1) Eneo linalohusu Sakramenti ya Ekaristi.
(2) Eneo linalohusu Sakramenti ya Upakwa Mafuta (Ordination), na
(3) Eneo linalohusu Utawala wa Kanisa (Magisterium) ambao unakabiliwa na jukumu na mamlaka ya kufundisha na kuhifadhi Imani.
SAKRAMENTI, ISHARA WAZI
Maeneo mawili ya kwanza kati ya maeneo matatu yaliyobaki yanahusu swala
la Sakramenti. Kwa kadiri ya Katekisimu yetu Sakramenti imeelezwa kuwa
ni “ISHARA WAZI”.
Kwa maana hiyo, swali linalotukabili sasa ni
hili: Je, jambo hili la “Ishara wazi” linaendana na Mungu wetu wa pekee
wa kweli ambaye Kristo Neno la Mungu ametufumulia katika Yn.8:26 kuwa ni
kweli?
Ili tuweze kuwa katika hali ya kulikabili swali hili
ipasavyo, sharti kwanza tujue uhalisia wa huyu Mungu wa pekee wa kweli,
na uhalisia wetu sisi watu wake.
Injili ya Kristo Neno la Mungu
ambayo imetimilika katika Nyaraka za Mitume, hutuambia kwamba Mungu ni
Roho (Yn.4:24) aliye Umoja wa Nafsi Tatu zisizogawanyika 1Yon.5:7
(Biblia Ndogo ya Agano Jipya) na kwamba, kutokana na hali yake hiyo,
awatafuta watu wamwabuduo katika Roho na Kweli (Yn.4:23).
Hivyo,
kwa kusimamia Yn.8:26 na 1Yn.5:7 Biblia ndogo ya Agano Jipya, Mungu ni
“Kweli” aliye Roho katika Umoja wa Nafsi Tatu, Kweli, na Neno, na Roho
Mtakatifu.
JE, MTU NI NANI?
Kuhusu mtu, Bibilia hutuambia
kwamba mtu ni nafsi kwa mfano na sura yake huyu Mungu aliye Nafsi Tatu
(Mw.1:26), na kwamba yeye ni wa kuhuishwa kwa Pumzi (Roho) ya Mungu na
kuumbiwa mwili wa nyama kutokana na mavumbi ya ardhi kuwa maskani yake
hapa duniani (Mw.2:7).
Hivyo, mtu halisi ni nafsi (utu wa ndani) anayekaa katika mwili wa nyama hapa duniani.
Kwa kushirikishwa kwake Pumzi (Roho) ya Mungu, mtu amejumuishwa katika
Umoja wa Nafsi Tatu, kwamba mtu ndani ya Mungu na Mungu ndani ya mtu
(1Hoh.4:13); na hivyo kuwa mshirika wa utimilifu wote wa Mungu
(Efe.3:19); na hivyo, kushiriki uhalisia ule ule wa Mungu, hapa duniani
(1Yoh 4:17).
Hivyo, kiuhalisia, mtu halisi au mtu wa ndani
(2Kor.4:16), ni nafsi kama alivyo Muumba wake, ni wa ulimwengu wa Roho,
ni wa ulimwengu wa mbinguni (Fil.3:20); yuko nje ya milango ile mitano
ya fahamu za kimwili wa nyama, yaani kuona, kusikia, kuonja, kunusa na
kuhisi. Hii ni milango ya fahamu katika maisha yetu ya Ulimwengu huu wa
mwili wa nyama hapa duniani tunapoishi kama wageni (1Pet.1:17); na siyo
katika maisha yetu ya utu halisi, nafsi katika Umoja wa Nafsi Tatu za
Mungu Kweli tulikojuishwa kwa kushirikishwa Roho wa Mungu (Yoh.4:13).
Kutokana na ukweli huu, mahusiano na mawasiliano kati yetu na Mungu
wetu wa kweli yanapaswa kuwa kwa jinsi alivyo Yeye aliye Roho; wala
hayapaswi kuendeshwa kwa akili za kimwili wa nyama (Kol.2:18).
Hivyo, Ndivyo Mungu alivyotuumba tuenende (Efe 2:10). Shetani akaja,
katutaperi, akatuua na kuharibu mpango wa Mungu kwa ajili yetu. Kristo
Neno la Mungu akaja kutufanya tuwe na uzima tena (Yon 10:10). Mungu
akatuhuisha tena, akatufufua na kutuketisha pamoja na Kristo Neno la
Mungu katika ulimwengu wa Roho (Kol.2:13-15; Efe 2:5-6).
Hivyo,
lile agizo la kututakatwende kwa Roho ni agizo linalotutaka sisi
tuliokombolewa na kuokolewa twende kwa kadiri ya uhalisia wa Mungu wetu
aliye Roho na anayetafuta watu wamwabudu katika Roho na Kweli kwa kuwa
Yeye ni Roho (Yn.4:24).
JE, UTARATIBU WA KWENDA KIROHO UKOJE?
Katika kutufundisha kuhusu swala hili, siku moja Yesu alimwuliza Yule
Ofisa, “Msipoona ishara na maajabu hamtaamini kabisa (Yn.4:48)? Tena,
ona alivyomwambia Mtume Toma, “Wewe kwa kuwa umeona, umesadiki. Wa heri
wale wasioona wakasadiki (Yn.20:29). Na kinyume cha “heri” ni “Ole”.
Kwa kauli hiyo tunaambiwa, “Ole wao wale wanaotaka waone ndipo
wasadiki”.
Katika kutimiliza Injili ya Kristo Neno la Mungu,
Nyaraka za Mitume kwanza hututafsiria neno imani; kwamba ni kuwa na
hakika ya mambo yatarajiwayo; ni bayana ya mambo yasiyoonekana
(Ebr.11:1).
Tunaambiwa katika Ebr.11:6 kwamba pasipo imani
haiwezekani kumpendeza Mungu; maana yeye amwendeaye Mungu sharti aamini
kwamba Yeye yuko, na kwamba huwapa thawabu wale wamtafutao. Katika
Ebr.10:38 Mungu anasema, “Mwenye haki wangu ataishi kwa imani; naye
akisitasita, Roho yangu haina furaha naye”.
Katika Yak.1:6-8
tunasoma, “Ila na aombe kwa imani pasipo shaka yoyote. Maana mwenye
shaka ni kama wimbi la bahari lililochukuliwa na upepo na kupeperushwa
huku na huku. Na mtu kama huyo asidhani ya kuwa atapokea kitu kwa
Bwana. Mtu wa nia mbili husitasita katika njia zake zote”.
Tunaambiwa katika 2Kor.5:7; “Twaenenda kwa imani; si kwa kuona”. Na
katika Gal.5:4-5 tunaambiwa, “Mmetengwa na Kristo ninyi mtakao
kuhesabiwa haki kwa sheria. Mmeanguka na kutoka katika hali ya neema
(aliyotustahilia Mungu katika Kristo Neno la Mungu pale Msalabani).
Maana sisi kwa Roho tunalizamia tumaini la haki kwa njia ya imani”.
Hivyo, sisi watu, kwa kuwa utu wetu halisi, nafsi, ni wa uhalisia wa
Mungu pekee wa Kweli ulio nje ya milango ya fahamu za kimwili wa nyama,
mahusiano na mawasiliano na Mungu wetu wa pekee wa kweli ni siri kati ya
Mungu na mtu kwa njia ya imani; ni siri kati ya Umoja wa Nafsi Tatu na
utu wa ndani, nafsi, iliyo utu halisi ihuishwayo kwa Roho wa Mungu
iliyotiwa ndani ya mtu husika.
Kwa mantiki hii, ibada za
kisakramenti na kivisakramenti ni ibada zilizo kinyume kabisa cha
uhalisia na mapenzi ya Mungu. Tena, kwa kweli, ni ibada adui dhidi ya
Mungu wa kweli anayetafuta kuabudiwa katika Roho na kweli. Hizi ni
ibada za kumwabudu mungu mwingine na zinazoenendwa na yesu mwingine
(2Kor.11:4). Kumwamini au kutomwamini Mungu itakiwavyo, ni swala la
kibinafsi. Hakuna kufanyiana. Ndiyo maana ni siri kati ya mtu na Mungu
katika kumkaribia Mungu kwa moyo wa kweli na utimilifu wa imani
(Ebr.10:22). Izingatiwe kwamba neno “Imani” ni kwa kadiri ya tafsiri ya
Ebr.11:1 na si vinginevyo. Si swala la kuamini yaliyotengenezwa na
wakubwa fulani (Kol.2:8-10), au yale mtu anayojitengenezea mwenyewe kwa
akili zake za kimwili wa nyama au nafsi yake.
ENEO LA UTAWALA WA KANISA
Eneo nyeti la tano lililobainishwa katika kifungu cha 79 cha “”Ut Unum
Sint” ni lile eneo linalohusu Utawala wa Kanisa (Magisterium) ambao
unakabiliwa na jukumu na mamlaka ya kufundisha na kuhifadhi imani.
Kuhusu eneo hili, hebu tuanze na Yn.6:45, Andiko ambalo hutuambia
kwamba watu wote watakuwa wamefundishwa na Mungu. Na Yn.14:26 Yesu
hutuambia kwamba Roho Mtakatifu Msaidizi atatufundisha yote na
kutukumbusha yote. Tena huyo Roho wa kweli atatuongoza na kututia
kwenye kweli yote, (Yn.16:13). Na 1Kor.2:10-12 hutueleza wazi kwamba
Mungu ametufunulia sisi kwa Roho. Maana Roho huchunguza yote hata
mafumbo ya Mungu. Maana ni nani katika binadamu ayajuaye mambo ya
binadamu ila roho ya binadamu iliyo ndani yake? Vivyo hivyo na mambo ya
Mungu hakuna ayafahamuye ila Roho wa Mungu. Lakini sisi hatukuipokea
roho ya dunia, bali Roho atokaye kwa Mungu tupate kuyajua tuliyokirimiwa
na Mungu.
Ndiyo maana nimesema hili swala la mahusiano na mawasiliano kati ya Mungu na mtu ni siri kati ya Mungu na mtu.
Katika Mt.23:8-10 Kristo Neno la Mungu anaweka yote pamoja, “Bali ninyi
msiitwe Rabi, maana Mwalimu wenu ni mmoja, nanyi nyote ni ndugu. Wala
msimwite mtu baba duniani, maana Baba yenu ni mmoja aliye wa mbinguni
(wa uhalisia wa Roho). Wala msiitwe viongozi, maana kiongozi wenu ni
mmoja naye ndiye Kristo”.
Kwamba, swala hili la mahusiano kati ya
Mungu na mtu ni la kila mtu binafsi limetabiriwa na manabii. Katika
Yer.31:33-34 Mungu aliahidi, “Nitatia sheria yangu ndani yao, na katika
mioyo yao nitaandika; nami nitakuwa Mungu wao nao watu wangu. Wala
hawatamfundisha mtu na jirani yake, na kila mtu na ndugu yake wakisema,
Mjue Bwana; kwa maana watanijua wote, tangu mtu aliye mdogo miongoni
mwao; hadi aliye mkubwa miongoni mwao maana nitausamehe uovu wao, wala
dhambi yao sitaikumbuka tena”.
Na kwa unabii wa Ezekiel Mungu
alisema, “Nami nitawanyunyizia maji safi, nanyi mtakuwa safi;
nitawatakaseni kutoka kwa uchafu wenu wote, na kutoka kwa vinyago vyenu
vyote. Nami nitawapa ninyi moyo npya, nami nitatia roho mpya ndani
yenu, nami nitatoa moyo wa jiwe uliomo ndani ya mwili wenu, nami
nitawapa moyo wa nyama. Nami nitatia roho yangu ndani yenu, na
kuwaendesha katika sheria zangu, nanyi mtazishika hukumu zangu na
kuzitenda (Eze.36:25-27).
Utabiri huu ndio ule ulioelezwa ya Yesu
mwenyewe kama tulivyoona hapo juu katika Mt.23:8-10, na kutimilizwa
kama ulivyoelezwa katika 1Kor.12:13; Gal.3:27 na ule upakwaji mafuta
ulioelezwa katika 1Yoh.2:20, 27. Aya hizo za mwisho zatuambia, “Ninyi
mmepakwa mafuta na Yeye aliye Mtakatifu nanyi mnajua nyote. Nanyi
mafuta yale mliyoyapata kwake yanakaa ndani yenu, wala hamna haja ya mtu
kuwafundisha; lakini kama mafuta yake yanavyowafundisha habari za mambo
yote, tena ni kweli wala si uongo, na kama yalivyowafundisha, kaeni
ndani yake”.
Upakwa mafuta na Roho Mtakatifu ulitabiriwa kama
ahadi katika nyakati za manabii, sasa katika nyakati timilifu unaelezwa
kwamba umetimilika kama tunavyohakikishiwa katika Nyaraka za Mitume
zilizo utimilifu wa Injili ya Kristo Neno la Mungu.
MASWALI YA KUJIULIZA NA MAJIBU YAKE
Ndipo tunapokuwa na haki ya kujiuliza:
Je? Maeneo haya ya ishara Wazi na Utawala wa Kanisa kama yalivyo
kiuhalisia, hayaendi kwa injili nyingine iliyo tofauti na ile
waliyoihubiri Mitume (Gal.1:8-9) na hivyo kuenenda na injili iliyo
laaniwa inayotupeleka kwa yesu mwingine na roho nyinginezo mbali na Roho
wa Kweli (Kor.11-4)?
MATENDO AU MATUNDA NDIYO DIRA
Tumeamriwa na kuonywa “Wapenzi msiiamini kila roho, bali zipimeni hizo
roho, kama zimetokana na Mungu, kwani kuna Roho wa kweli na roho ya
upotevu (1Yon.4:1, 6).
Tena tumeagizwa, “Ufanyeni mti kuwa mzuri
na matunda yake kuwa mazuri. Au ufanyeni mti kuwa mbaya na matunda yake
kuwa mabaya, kwa maana kwa matunda yake mti hutambulikana. Enyi wazawa
wa nyoka, mwawezaje kunena mema mkiwa wabaya? Maana kinywa cha mtu
huyanena yaujazayo moyo wake. Mtu mwema katika akiba njema hutoa mema;
na mtu mbaya katika akiba mbaya hutoa mabaya (Mt.12:33-35) Mtawatambua
kwa matendo yao (Mt.7:16, 20).
Tumeagizwa, “Basi nasema Nendeni
kwa Roho, wala hatazitimiza kamwe tamaa za mwili. Kwa maana mwili
hutamani kushindana na Roho, na Roho kushindana na mwili; kwa maana hizi
zimepingana, hata hamwezi kufanya mnayotaka (Gal.5:16-17).
Matendo ya kwenda kwa mwili yameorodheshwa na Paul Mtume katika
Gal.5:19-21 kuwa ni: Uasherati, uchafu, ufisadi, ibada ya sanamu,
uchawi, uadui, ugomvi, wivu, hasira, fitina, mafarakano, uzushi, husuda,
ulevi, ulafi na mambo yanayofanana na hayo, katika hayo nawambia mapema
kama nilivyokwisha kuwaambia, ya kwamba watu wayatendao mambo ya jinsi
hiyo, hawataurithi ufalme wa Mungu.
Tena twaambiwa, “Mambo hayo
yanaonekana kana kwamba yana hekima katika namna ya ibada mliyojitungia
wenyewe na katika kunyenyekea, na katika kuutawala mwili kwa ukali;
lakini hayafai kitu kwa kuzizuia tamaa za mwili (Kol.2:23).
Twaangalishwa, “Angalieni mtu asiwafanye mateka kwa elimu yake ya bure
na madanganyo matupu, kwa jinsi ya mapokeo ya wanadamu, kwa jinsi ya
mafundishao ya awali ya ulimwengu, wala si kwa jinsi ya Kristo. Maana
katika Yeye unakaa utimilifu wote wa Mungu, kwa jinsi ya kimwili. Na
ninyi mmetimilika katika Yeye aliye kichwa cha enzi yote na mamlaka
(Kol.2:8-10).
Pia, tunatakiwa tupate utajiri wote wa kufahamu kwa
hakika, tupate kujua kabisa siri ya Mungu yaani Kristo; ambaye ndani
yake Yeye hazina zote za hekima na maarifa zimesitirika (Kol.2:2-3).
Kiuhalisia katika maeneo haya matatu, kunakosekana kabisa jitihada za
kuwasaidia wadau wa kanisa kufahamu kwa hakika, wapate kujua kabisa siri
ya Mungu, yaani Kristo.
Ndipo tunapoambiwa kwamba tunda la
kwenda kwa Roho ni lile lilioodheshwa katika Gal.5:22-23; na katika
Gal.5:4-5 twasoma, “Mmetengwa na Kristo ninyi mtakao kuhesabiwa haki kwa
sheria. Mmeanguka na kutoka katika hali ya neema. Lakini sisi kwa
Roho twalitazamia tumaini la haki kwa njia ya Imani”.
MUHTASARI WA MAENEO MATATU YA MWISHO KATI YA YALE MATANO
Baada ya maagizo, maamuru maelekezo maangalisho tuliyoyapewa na Neno la
Mungu tunahitimisha ukweli kwamba yale maeneo mawili ya kiishara wazi
yako nje ya Kristo na Mungu wa pekee wa kweli anayetaka kuabudiwa katika
Roho na kweli.
Na lile eneo la Utawala wa Kanisa nalo liko nje
ya Kristo Neno la Mungu kwa sababu kanisa linalohusika na Utawala huu ni
kanisa la kimwili na imani inayofundishwa ni ile inayosemekana katika
ile sala ya Imani “Mungu wangu nasadiki ninayofunashwa kusadiki na
Kanisa Katoliki la Roma; kwani ndiwe uliyefumbulia hayo. Imani hii iko
nje kabisa na ile imani iliyotafsiriwa katika Ebr.11:1 na kusisitizwa
katika aya nyinginezo nyingi za Biblia.
Hiki kipengele “Ndiwe uliyefundulia hayo….” Hakizingatii ukweli kwamba:-
(1) Yupo yule mwasi na mpingamizi ajiinuaye nafsi yake juu ya kila
kiitwacho mungu ama cha kuabudiwa, hata yeye mwenyewe kuketi katika
hekalu la Mungu akijionesha nafsi yake kana kwamba yeye ndiye Mungu
(2Thes.2:4).
(2) Ipo roho ya upotevu (1Yon.4:6) ambayo iko kazini
kuwapoteza watu wasiijue kweli wasije wakamwongokea Mungu wa kweli
akawaponya (2Kor.4:3-4; Yn.12:40).
Na kutokana na dira
tuliyoipewa kupimia roho, hali yakushamiri madhambi hata ndani ya wana
makanisa, ni kithibiti tosha kwamba roho ya upotevu ndiyo inayoshikilia
makanisa na kupofusha wana makanisa wasichomoke kutoka gereza na
minyororo ya utumwa wa dhambi. Mfalme wa Uwezo wa anga, roho Yule
atendaye kazi sasa katika wana wa kuasi ndiye anayetawala, makanisa.
Hivyo, maeneo matatu yaliyotubakia yako katika uadui dhidi ya Mungu wa pekee wa kweli. Ipo haja ya kujitoa katika hali hii.
MAENEO HAYA MATATU YAKO KINYUME CHA “UT UNUM SINT”
Katika kifungu Na.1 cha Barua yake ya Kichungaji “Ut Unum Sint”, Mt.
Papa Yohani Paulo II anatoa hamasa ya kupambana na mwelekeo wa dunia ya
kufuta kabisa nguvu za Fumbo la Ukombozi. Katika kifungu hicho, Papa
amewataka waamini Kristo kuuishi UKWELI mmoja kuhusu Msalaba, kinyume
cha dunia inayokana ukweli kwamba katika Msalaba mtu ana chimbuko la
uzima mpya. Dunia hudai kwamba Msalaba hauwezi kumpa mtu maono wala
matumaini. Dunia husema kwamba mtu si chochote bali ni kitu cha
kiudongo tu kinachopaswa kuishi kana kwamba Mungu hayupo.
Kwa
kwenda kimwili wa nyama kama inavyothibitika katika maeneo haya matatu,
makanisa yetu siyo tu kwamba yanaelekea, bali kiuhalisia, yanakanusha
nguvu ya Fumbo la Ukombozi pale Msalabani. Kiuhalisia, makanisa yetu
hayatambui Fumbo la Ukombozi ulio katika Kristo Yesu ambaye Mungu
amekwisha kumweka awe upatanisho kwa njia ya imani katika damu yake, ili
aoneshe haki yake, kwa sababu ya kuziachilia katika ustahimili wa Mungu
dhambi zote zilizotangulia kufanywa (Rumi 3:24-25). Makanisa
hayatambui kwamba Mungu ametupatanisha sisi na Nafsi yake kwa Kristo
pale Msalabani; yaani Mungu alikuwa ndani ya Kristo akiupatanisha
ulimwengu na Nafsi yake asiwahesabie makosa yao. Kwamba Yeye asiyejua
dhambi alimfanya kuwa dhambi kwa ajili yetu, ili sisi tupate kuwa haki
ya Mungu katika Yeye (2Kor.5:18-19, 21).
Kwa kutotambua ukweli
huu wa wema, huruma, upendo, uwezo na namna za Mungu (Isa.55:8-13)
makanisa hujitungia ibada na taratibu zao za kuhusiana na kuwasiliana na
Mungu ambazo hazifai kitu kwa kuzizuia tamaa za mwili (Kol.2:23;
Gal.5:19-21). Matokeo yake watu hubaki kuwa watumwa wa dhambi. Na
Mungu hawasikii wenye dhambi (Yn.9:31). Ndiyo maana kuna kutengwa na
Kristo, kuanguka na kutoka katika hali ya neema. Iliyobaki ni
kutourithi ufalme wa Mungu (Gal.5:4-5, 21; Ebr.10:26-27, 29). Kwa
kutoenenda kwa Roho, makanisa hushiriki 100% ile dhambi ya kupuuza
kilichofanyika pale Msalabani.
SASA MCHAWI WETU NI NANI?
Basi
niseme nini juu ya hayo? Kifupi, tumtambue mchawi wetu. Naye si
mwingine, bali ni shetani. Kumtafuta mchawi mwingine nje ya Shetani ni
kupoteza muda na mwelekeo. Tumeambiwa, “Hata hamwezi kufanya mnayotaka
(Gal.5:17). Nafsi wewe ni nafsi tegemezi: Au kuungana na Kweli au
Ibilisi. Wewe kama wewe, au mimi kama mimi, sote hatuwezi kufanya
tunayotaka (Gal.5:17).
Ukihama dini au ukianzisha dini, ibilisi
atakukuta huko huko. La kufanya tumekwisha kuambiwa katika 1Kor.7:20 na
24, “Basi ndugu zangu, kila mtu na “akae mbele za Mungu”, pale pale
alipo. Hakikisha unakaa mbele za Mungu wa pekee wa kweli hapo hapo
ulipo.
Tunaukumbuka usemi wa Papa Yohani Paulo II, Kifungu cha 80
cha “Ut Unum Sint” kwamba wote, kuanzia Maaskofu hadi waamini walei,
wamepokea Upako wa Roho Mtakatifu. Tumeona matokeo ya kupokea Upako
Mtakatifu ni kuingiwa na Roho Mtakatifu anayekaa ndani ya mtu
kumfundisha kweli yote na kumwongoza mtu na kumtia kwenye kweli yote.
La kufanya ni moja tu; nalo ni kuhakikisha unakaa mbele za Mungu wa
pekee wa kweli, kwa Neno lake yaani Roho wake anayekutamani kiasi cha
kuona wivu (Yak.4:5). Yeye atakunong’oneza siri yake yote (1Yon.2:20,
27). Kaa katika Neno lake (Yn.8:31-32). Hicho ndicho chakula kitiacho
uzima (Yn.6: 63), tena uzima tele (Yn.10:10).
Amani yake Kristo
Neno la Mungu, amani ile aliyoisema katika Yn.14:27, itamalaki ndani
yako na kati yetu katika kuukulia ukweli wa Mungu kwa sifa na Utukufu wa
huyu Mungu wetu wa pekee wa kweli, na kwa uzima na usalama wetu.
Na ubarikiwe kwa Baraka zote za kiroho katika ulimwengu wa roho ndani yake Kristo Neno la Mungu (Efe.1:3) sasa na hata milele.
LUKA ROKI MAGHALI CHAMAYOMBE
0787 765 759
0714 118 428
0753 298 707
Chamayombe37@gmail.com
Subscribe to:
Post Comments (Atom)



0 comments:
Post a Comment