Tumepata kujua kwa uhakika kwamba:
Mungu wetu ni Roho (Yn.4:24) aliye katika Umoja wa Nafsi Tatu ambazo ni Kweli, na Neno na Roho Mtakatifu.
Mbinguni anakokaa huyu Mungu ni huu Umoja wa Nafsi Tatu, na
Ufalme wake ambao ni wa haki, amani na furaha katika Roho Mtakatifu (Rum.14:17), umeundwa na huu huu Umoja wa Nafsi Tatu.
Baada ya kujua kweli hizi, sasa tutendeje?
Kabla ya yote, tunapaswa kufahamu kabisa kwamba shida au tatizo
linalotukabili ambalo linahitaji kushughulikiwa ni lile kosa
tulilolirithi kutoka kwa wazazi wetu wa kwanza, Adamu na Eva. Kosa
lenyewe ni lile tendo la kumwamini Ibilisi na kumfanya Mungu wa pekee wa
Kweli kuwa mwongo (Mw.2:16-17; 3:4-5).
Katika hili, Mdo.2:38
humnukuu Petro Mtume akisema, “Tubuni mkabatizwe kila mmoja kwa Jina
lake Yesu Kristo, mpate ondoleo la dhambi zenu, nanyi mtapokea kipawa
cha Roho Mtakatifu”.
Petro Mtume amesema, “Tubuni mkabatizwe……….”
Kubatizwa ni kufanywaje? Kwa kadiri ya 1Kor.12:13, kubatizwa ni
kunyweshwa Roho Mtakatifu. Na kwa kadiri ya 1Yoh.4:13, hushirikishwa
Roho wa Mungu ndio huko huko kubatizwa. Na kwamba kwa tendo hilo, mtu
huwa ndani ya Mungu ambaye ni Roho mwenye Nafsi Tatu, na Mungu Roho
mwenye Nafsi Tatu naye huwa ndani ya mtu husika. Kwa tendo hilo mtu
husika huwa ameingizwa na kujumuishwa katika Umoja wa Nafsi Tatu za
Mungu wa pekee wa Kweli.
Kwa tendo la Ubatizo huo katika Roho
Mtakatifu, Mungu wa pekee wa Kweli amejibu 100% lile ombi alilowaombea
watu wake siku moja kabla ya kusulubiwa kwake (Yn.17:21-23). Kwa
ubatizo huo, wahusika wamezaliwa mara ya pili kwa Neno la Munu lenye
uzima lidumulo hata milele (1Pet.1:23). Kwa Ubatizo huo wahusika
wamehuishwa au kufufuliwa na kuketishwa pamoja na Kristo katika
ulimwengu wa Mungu Roho aliye katika Umoja wa Nafsi Tatu (Efe.2:5-6;
Kol.2:13-15).
Kwa ubatizo katika Roho Mtakatifu, wahusika
wamezaliwa kwa Neno la Mungu lenye uzima lidumulo hata milele. Lakini
“Neno la Mungu” ndilo Jina halisi la Kristo Yesu, Jina ambalo, kwa
kadiri ya Ufu.19:12-13, lilikuwa siri ya Mungu. Jina ambalo
lilidhihirishwa na Yesu mwenyewe (Yn.17:6, 26), na ambalo, kwa kadiri ya
Mdo.4:12, ndilo Jina pekee tulilolipewa wanadamu litupasalo sisi
tuokolewe kwalo, kama tulivyoona katika 1Pet.1:23.
SHARTI LA UBATIZO HUO NI KUTUBU
Petro Mtume alisema, “Tubuni mkabatizwe…..” Kwa maana kwamba sharti la
kubatizwa ni “kutubu”. Kwamba ili mtu apate kubatizwa, sharti atubu.
Na kutubu si swala la kutamka maneno tu. Mbona hilo hata kasuku
hulifanya wakizoezwa. Kutubu ni tendo la kufanya kinyume kabisa cha
kosa lililofanywa. Kutubu ni kufanya mapinduzi dhidi ya kosa.
KOSA MAMA NI LIPI?
Ni kwamba baada ya kujiumbia mtu wake awe nafsi kwa mfano na sura yake
Yeye mwenyewe aliye Roho mwenye Nafsi Tatu zilizo Umoja, hata
kumshirikisha Pumzi au Roho wake atiaye uzima (Mw.1:26; 2:7; Yn.6:63),
Mungu alimwagiza mtu wake jinsi ya kuenenda.
Agizo lilikuwa
kwamba asile matunda ya mti wa ujuzi wa mema na mabays; kwa tahadhari
kwamba siku atakayokula matunda ya mti huo atakufa hakika (Mw.2:17).
Ibilisi katika umbo la nyoka, akamkanushia Eva kwa kumwambia, “Hakika
hamtakufa, kwa maana Mungu anajua ya kwamba siku mtakayokula matunda ya
mti huo, mtafumbuliwa macho, nanyi mtakuwa kama Mungu mkijua mema na
mabaya” (Mw.3:4-5).
Eva na Adamu wakawa wameshawishika kumwamini na kumtii shetani, na kumfanya Mungu mwongo hata kumwasi kabisa.
Hiyo ndiyo dhambi mama hapa duniani. Kwamba shetani ndiye wa kuaminiwa
na kumtii. Na kwamba Mungu si wa kuaminiwa wala kumtii, kwa sababu ni
mwongo.
Sasa, ili apate ubatizo uliosemekana hapo juu, mtu
anatakiwa kufanya mapinduzi. Sharti amwamini Yeye (Neno la Mungu)
aliyetumwa na Yeye (Kweli, Mungu Baba) (Yn.6:27); na kuachana kabisa na
Yule muuaji ambaye hasimami katika kweli Yule mwongo aliye baba wa
uongo. Mapinduzi hayo ndiyo kutubu; ndiyo toba ya kweli.
Lakini
ili kubatizwa katika Roho Mtakatifu, ili kunyweshwa Roho Mtakatifu
kunahitajika toba ya kina, siyo ya kijuujuu tu. Toba ya kina ni ile ya
kumkaribia Mungu katika hali ya kuwa mkweli 100% kwa imani ya 100%
kwamba umenyunyiziwa Damu ya Yesu, uachane na dhamiri mbaya. Uache
kuhukumiwa na moyo wako; maana Nafsi yako imeoshwa kwa maji safi na hai
yaliyomo katika Damu ya Yesu, Roho Mtakatifu ambaye yumo katika Neno la
Mungu, Krito Yesu (Ebr.10:19-22).
Tumehamasishwa kulishika sana
ungamo la tumaini letu lisigeuke; maana Yeye aliyeahidi kwa kusema, “Hii
ndiyo Damu yangu ya agano imwagikayo kwa ajili ya wengi, Yeye aliyahidi
kwa kusema, “Dhambi zao na uasi wao sitaukumbuka tena kabisa, ni
mwaminifu wala hakuna uongo wowote ndani yake (Ebr.10:23; 1Yoh.2:21).
HITIMISHO
Kwa maelezo hayo yote jibu la swali lile “Tutendeje ndugu zetu?” Ni moja, nalo ni:
“HUU MWENENDO WA KUMFANYA MUNGU WA PEKEE WA KWELI KUWA MWONGO UKOME KWA
KILA MMOJA WETU” Badala yake tutubu kwa maana iliyoelezwa hapo juu; na
katika msingi wa kweli ya 100%, kila mmoja wetu, hata wewe hapo, awe na
amani ya 100% na Mungu wetu wa pekee aliyefaulu 100% kuondoa tatizo la
utumwa wa dhambi lililokuwa linatukabili na ambalo linakwamisha Uhalisia
wa Ufalme wa Mungu duniani kwa hasara ya kila mhanga wa Ibilisi. Wote
kwa sauti moja tuseme, “Kosa la kutomwamini Mungu Kweli, Roho aliye
katika Nafsi Tatu, sasa BASI!!!” Na hivyo, kila mmoja wetu binafsi, kwa
nafsi yake yote, kwa akili yake yote na kwa nguvu ya Roho Mtakatifu
itendayo kazi ndani yake aamini 100% kwamba pale Msalabani kazi
imekwisha. Sasa yuko safi, na hakuna wa kumshitaki wala kumhukumu kwa
lolote lile (Rum.8:31-39). Kila mmoja wetu awe na amani sawasawa na
Neno la Mungu Rum.5:1.
Furahia Baraka unazobarikiwa na Mungu wa pekee wa kweli sasa hata na milele.
LUKA ROKI MAGHALI CHAMAYOMBE
0787 765 759
0714 118 428
0753 298 707
Chamayombe37@gmail.com
Subscribe to:
Post Comments (Atom)



1 comments:
Neno zuri sana kutoka kwako, Mzee Chamayombe. Mungu akubariki sana ili uendelee kutuletea Neno la Mungu!
Post a Comment