Katika kifungu cha 79 cha Barua yake ya Kichungaji “Ut Unum Sint” Mt.
Papa Yohani Paul II anatubainishia maeneo matano ambayo yanahitaji
kujifunzwa kwa ukamilifu zaidi.
Maeneo hayo ni:-
(1)
Mahusiano kati ya Maandiko Matakatifu kama Mamlaka ya juu kuliko yote
katika maswala ya imani, na Mapokeo Matakatifu kama si ya kupuuzwa na
kuwekwa kapuni katika kufafanua Neno la Mungu.
(2) Ekaristi kama
Sakramenti ya Mwili na Damu ya Kristo. Toleo la sifa kwa Baba,
kumbukumbu la Sadaka na uwepo halisi wa Kristo na Miminiko litakasalo la
Roho Mtakatifu.
(3) Upakwa Mafuta (Ordination) kama Sakramenti ya
kumtoa mtu kwenye ulei kumwingiza kwenye Ukleri kwa huduma za ibada za
kikanisa.
(4) Utawala wa Kikanisa Uliodhaminishwa kwa Papa na
Maaskofu walio Umoja naye. Utawala huo waeleweka kama wajibu na
mamlaka, itekelezwayo katika Jina la Yesu kwa madhumuni ya kufundisha na
kulinda imani.
(5) Na mwisho kuna swala la Mama yetu Bikira Maria, ambalo tumekwisha kulipitia.
SWALA NA.1
Katika kushughulikia Swala Na.1 ni muhimu tujue kwamba Injili ya Kristo
Neno la Mungu inamhusu Yeye mwenyewe katika kuja kwake awe Nuru ya
Ulimwengu ili kila amwaminie na kumfuata asikae gizani, bali awe na
uzima wa milele (Yn.8:12; 12:46). Kwamba amekuja aupe ulimwengu akili
kwamba umjue Yeye aliye Mungu wa kweli na uzima wa milele (1Yoh.5:20).
Na Mapokeo Matakatifu, kama inavyosemekana katika vifungu 17 na 78 vya
“Ut Unum Sint”, ni mafundisho na/au Mahubiri ya Mitume yanayotufikia kwa
njia ya Nyaraka zao.
YESU ALIWAAMBIA NA KUWAFANYIA NINI MITUME?
Katika Lk.10:16, Bwana Yesu aliwaambia Mitume, “Awasikilizaye ninyi,
anisikiliza mimi; naye awakataaye ninyi,anikataa mimi; naye anikataaye
mimi, amkataa Yeye aliyenituma”.
Tena akasema “Yeye ampokeaye mtu yeyote nimtumaye, anipokea mimi; naye anipokeaye mimi, ampokea Yeye aliyenituma” (Yn.13:20).
Katika Yn.14:15-18, Kristo Neno la Mungu akawaambia Mitume, “Mkinipenda
mtazishika amri zangu. Nami nitamwomba Baba, Naye atawapa Msaidizi
mwingine, ili akae nanyi hata milele; Ndiye Roho wa Kweli. Sitawaacha
ninyi yatima; naja kwenu”.
Akaendelea kusema katika Yn.14:26
“Lakini huyo Msaidizi, huyo Roho Mtakatifu ambaye Baba atamtuma kwa Jina
langu, atawafundisha yote na kuwakumbusha yote niliyowaambia”.
Na katika Yn.16:12-14 akawaambia, “Hata bado ninayo mengi ya kuwaambia,
lakini hamwezi kuyastahimili hivi sasa. Lakini Yeye atakapokuja, huyo
Roho wa Kweli atawaongoza awatie kwenye kweli yote; kwa maana hatanena
kwa Shauri lake mwenyewe, lakini yote atakayoyasikia atayanena, na mambo
yajayo atawapasha habari yake. Yeye atanitukuza mimi, kwa kuwa atatwaa
katika yaliyo yangu na kuwapasha habari.
Kauli hizi zote kwa pamoja zatuhakikishia kwamba mwanadamu kama mwanadamu katika uasili wake hawezi kufahamu kweli ya Mungu.
Ndiyo maana Kristo Neno la Mungu ametukataza tusikubali kuitwa walimu,
“Bali ninyi msiitwe Rabi, maana Mwalimu wenu ni mmoja, nanyi nyote ni
ndugu (Mt.23:8). Na katika Yn.6:45 “Imeandikwa katika manabii, Na wote
watakuwa wamefundishwa na Mungu. Basi kila aliyesikia na kujifunza kwa
Baba huja kwangu”.
KRISTO ATIMIZA AHADI YA KUWAOMBEA MITUME
Katika Yn.17:21-23 tunalisoma ombi: “Wote wawe na umoja, kama vile Baba
ulivyo ndani yangu nami ndani yako; hao nao wawe ndani yetu; ili
ulimwengu upate kusadiki ya kwamba wewe ndiwe uliyenituma. Nami utukufu
ule ulionipa nimewapa wao; ili wawe na umoja kama sisi tulivyo umoja.
Mimi ndani yao, Nawe ndani yangu, ili wawe wamekamilika katika umoja;
ili ulimwengu ujue ya kuwa ndiwe uliyenituma; ukawapenda wao kama
ulivyonipenda mimi”.
AHADI YA KUWAPA ROHO MTAKATIFU YATIMIZWA
Baada ya kukamilishwa kwa tendo la Ukombozi, na kuondolewa dhambi pale
Msalabani, siku kadhaa kupita baada ya kufufuka kwake, Yesu akawatokea
Mitume wake, akawaambia tena “Amani iwe kwenu; kama vile Baba
alivyonituma mimi, nami nawatuma ninyi. Naye akiisha kusema hayo,
akawavuvia, akawaambia, Pokeeni Roho Mtakatifu”.
Kwa tendo hilo
la kuwapa au kuwashirikisha Roho Mtakatifu, ikawa kwamba Mitume wako
ndani ya Mungu na Mungu ndani ya Mitume (1Yoh.4:13). Mitume wakawa
wamejumuishwa katika Umoja wa Nafsi Tatu za Mungu, Mitume wakawa Umoja
na Mungu. Mitume wakawa wamenyweshwa (1Kor.12:13) na kuvalishwa
(Gal.3:27) utimilifu wote wa Mungu (Efe.3:19). Kama vile Mungu wa pekee
wa Kweli alivyo, ndivyo walivyokuwa sasa Mitume ulimwenguni humu
(1Yoh.4:17). Wakawa tayari wamezaliwa mara ya pili (Yn.3:3) kwa Maji
hai ya Roho Mtakatifu (Yn.3:5; Yn.4:10, 14; 7:37-39). Wakawa wameuingia
rasmi ulimwengu wa Mungu wa pekee wa kweli, ulimwengu wa mbinguni,
ulimwengu wa Roho.
Hapo Mitume wakawa wamebakiwa na kazi moja tu.
Nayo ni kuukulia Umungu wa pekee wa Kweli (Pet.2:2) kwa kadiri ya
maongozi ya Roho Mtakatifu aliyekuwa ndani ya kila mmoja wao. Hapo kila
mmoja wao alikuwa ndani ya Mungu wa Pekee wa Kweli, na Mungu wa Pekee
wa Kweli alikuwa ndani ya kila mmoja wao, kwa huyo Roho Mtakatifu
aliyekuwa ndani ya kila mmoja wao. Hatima yake ni kwamba kila mmoja wao
alikuwa ndani ya kila mmoja wao, kwa huyo Roho Mtakatifu kuwa ndani ya
kila mmoja wao.
Na kwa kuwa Umoja wa Nafsi Tatu za Mungu wa Pekee
wa Kweli haugawanyiki kwa njia ya huyo Roho, kila mmoja wao alikuwa
ndani ya Umoja wa Utatu Mtakatifu na Umoja wa Utatu Mtakatifu ukawa
ndani ya kila mmoja wao. Hapo ndipo kila mmoja wao alipopata kutimilika
kwa utimilifu wote wa Mungu (Efe.3:19) hapa duniani (1Yoh.4:17).
Na kwa jinsi hii, yale Kristo Neno la Mungu aliyojisomea Mwenyewe
kuhusu kutumwa kwake (Lk.4:18); yakawa yametimilika 100% kwa Mitume.
Hivyo, mahusiano kati ya Injili na Mapokeo (Nyaraka za Mitume) ni
kwamba ile kazi ya Yesu kuwa Nuru ya Ulimwengu (Yn.8:12; 12:46) na
kutupatia akili ya kumjua Mungu wa pekee wa kweli (1Yoh.5:20),
imetimilikia katika Mapokeo Matakatifu au Nyaraka za Mitume. Bila
Nyaraka za Mitume, Injili ya Kristo Neno la Mungu haijatimilika, ina
mapungufu.
MADHARA YA KUPUUZA MAPOKEO MATAKATIFU
Hivyo,
kupuuza Nyaraka za Mitume au Mapokeo Matakatifu ni kujiamlia kubaki
gizani milele. Tena ni kumpuuza Kristo na Yeye aliyemtuma Kristo
(Lk.10:16), ni kumkufuru Roho Mtakatifu aliye Mtendaji Mkuu.
Kupuuza Mapokeo Matakatifu au Nyaraka za Mitume ni janga kuu la
kukomeshwa mara moja kwa sifa na Utukufuu wa Mungu wa pekee wa Kweli, na
kwa usalama wetu sisi watu wake aliojiumbia mwenyewe ambao Ibilisi
ametuteka kwa utaperi.
Wakati umefika wa kuondokana na laana
iliyosemekana katika Gal.1:8-9. “Lakini ijapokuwa sisi au malaika wa
mbinguni atawahubiria ninyi injili yoyote isipokuwa hiyo
tuliyowahubiria, na alaaniwe. Kama tulivyotangulia kusema, na sasa,
naseka tena, mtu awaye yote akiwahubiria ninyi injili yoyote, isipokuwa
hiyo mliyoipokea, na alaaniwe”.
Kwa nini ni laana kuhubiri injili
nyingine? Injili yoyote isiyo ile waliyoihubiri Mitume, injili yoyote
inayogongana na Injili walioihubiri Mitume, ina mapungufu. Hivyo,
injili yoyote inayogongana na Mahubiri ya Mitume inapelekea kumhubiri
Yesu mwingine na kuoenenda na maroho mengine mbali kabisa na Roho
Mtakatifu (2Kor.11:4).
KAULI YA MABABA WA KANISA
Katika
kifungu cha 100 cha Barua yake ya kichungaji “UT UNUN SINT” Mt. Papa
Yohani Paulo II amerejea Barua yake aliyokuwa amewaandikia Maaskofu,
Makleri na Waamini wa Kanisa Katoliki kuonesha njia ya kufuatwa katika
kuelekea kwenye Adhimisho la Yubilee Kuu ya Mwaka Mtakatifu 2000.
Katika Barua hiyo walengwa waliambiwa “Maandalizi bora kuliko yote kwa
elfu mpya yanaweza kuelezeka kwa ujitoaji uliopyaishwa katika kutumia
kiuaminifu kadiri iwezekanavyo Mafundisho ya Vatikani II katika maisha
ya kila mtu binafsi na katika Kanisa lote kwa ujumla.
Miongoni
mwa Mafundisho ya Vatikani II ni yale ambayo Baba huyu ametuambia katika
Barua yake hii hii “UT UNUM SINT” nayo ni: Kuwa waaminifu kwa Injili,
Kuiongokea Injili kwa kina, kuwa na fikra mpya, kuwa na mtazamo mpya wa
mambo (Kifungu cha 15). Kuiheshimu Kweli kuliko chochote kile kwa kuwa
Kweli ni Mungu (Kifungu cha 18).
Na katika kifungu cha 36, Baba
anatuambia kwamba katika mchakato wa kutafuta kweli, namna zote za
kuelezea imani zetu kamwe zisiwe kizingiti. Ukweli wote ambao Roho
Mtakatifu huwaongoza wanafunzi wa Kristo sharti Upokewe wote. Aina zote
za ujanjaujanja na makubaliano ya kirahisirahisi (ikiwa ni pamoja na
unafiki) lazima yaepukwe kabisa. Maswala nyeti sharti yatafutiwe
ufumbuzi, kwani vinginevyo, yatarudi tena wakati mwingine, au kwa namna
zile zile, au katika sura tofauti.
Hivyo ndivyo Mababa wa Kanisa
Katoliki wanavyotufundisha na kutuelekeza au kutuongoza. Hivyo ndivyo
Wachungaji wetu wakuu wanavyotuchunga. Basi, hivyo ndivyo Mahaba na
wachungaji wetu walio chini yao wanavyopaswa kutulea na kutuchunga.
Vinginevyo ndipo linaposimama lile neno, “Awasikilizaye ninyi,
anisikiliza mimi; naye awakataaye ninyi, anikataa mimi, naye anikataaye
mimi, amkataa Yeye aliyenituma”.
Kristo Yesu Neno la Mungu ndiye
Njia, kweli na Uzima (Yn.14:6). Tena ametuhakikishia kwamba Yeye ndiye
Mlango (Yn.10:7, 9) tena ndiye Mchungaji mwema (Yn.10:11, 14). Sasa,
yeyote Yule amkataaye Kristo kwa kuwakataa Mitume ameuingiaje huo ubaba
au uchungaji, na anamwakilisha Yesu yupi? Je, Siyo Yule Yesu mwingine
aliyesemekana katika 2Kor.11:4? Na kama ni hivyo, atabakia aendelee
kuwaangamiza watu wa Mungu mpaka lini? Tuwe waaminifu kwa Injili, na
kuiongokea Injili kwa kina!
HITIMISHO
Pengine kazi njema
anayoifanya Raisi John Magufuli katika kuisafisha Serikali na nchi ya
Tanzania ingekuwa mfano mzuri katika kusafisha Makanisa yetu. Na pia
katika kutekeleza jambo hili, mfano mwingine ni ule tunaoukuta katika
jeshi la Gideoni. Kati ya maaskari 32,000, askari walichujwa hata
wakabaki watu 300 (mia tatu tu). Na kwa idadi hiyo ndogo, Mungu
akajithibitishia ushindi wa kishindo (Amu.7:1 na kuendelea)..
Walatini walikuwa na msemo wao, “Non numerantur, sed ponerantur” kwamba
jambo la maana si idadi (jinsi wanavyohesabiwa, bali thamani (jinsi
wanavyothaminiwa). Au kwa Kiswahili, “wingi si hoja”. Ni bora kubaki
na wahudumu wachache chini ya Uongozi wa Mungu wa Kweli kuliko kuwa na
lukuki la wahudumu walio chini ya Yesu mwingine na maroho mengine.
Watambulikana kwa matendo yao (Mt.12:33).
Nuru ya Kristo ambayo
ilipangwa iufikie ulimwengu kwa njia ya Mapokeo Matakatifu au Nyaraka
za Mitume kamwe isiruhusiwe iendelee kukwamishwa kwa hoja au kisingizio
chochote kile. Nyaraka za Mitume ziheshimiwe 100%, kwani Injili ya
Kristo Neno la Mungu ndimo ilimotimilikia. Nje ya hapo ni kuenenda
kimapungufu na kutumbukia kuzimu kaburi la milele la nafsi zilizo nje ya
Umoja wa Nafsi Tatu za Mungu wa Pekee wa Kweli. Kilele cha kuufikia
Ukweli wa Mungu ni Nyaraka za Mitume.
Yote yakiwa kwa sifa na
utukufu wa Mungu wa pekee wa kweli, na kwa wokovu wa watu wa Mungu
wanaodidimizwa gizani au maangamizoni kwa upofushaji unaoendelea wa Yule
mwovu ibilisi (2 Kor.4:3-4; Yn.12:40).
Barikiwa Sana!!!
LUKA ROKI MAGHALI CHAMAYOMBE
0787 765 759
0714 118 428
0753 298 707
Chamayombe37@gmail.com
Subscribe to:
Post Comments (Atom)



0 comments:
Post a Comment