Katika kutafakari swala la imani, hebu tuanze na aya zifuatazo: Gal.5:16-17; Mk.10:27; 9:23 na Mt.17:20.
Gal.5:16-17 hutuambia, “Basi nendeni kwa Roho wala hamtazitimiza kamwe
tamaa za mwili. Kwa sababu mwili hutamani ukishindana na Roho, na Roho
kushindana na mwili, maana hizi zimepingana HATA HAMWEZI KUFANYA
MNAYOTAKA.
Nafsi ya mwanadamu ambaye ni mfano na sura ya Mungu,
aliye Nafsi Tatu, ilipata kuwa nafsi hai baada ya kushirikishwa uzima
halisi wa Mungu mwenyewe (Mw.2:7).
Hivyo, mwanadamu kama
mwanadamu ni nafsi isiyo na uhai wake mwenyewe. Na hivyo, katika hali
hiyo mwanadamu kama mwanadamu hawezi kufanya kitu.
Ndiyo maana,
katika Mk.10:27 Bwana Yesu Neno la Mungu, anasema “Kwa binadamu
haiwezekani”, kwani hana uhai wake mwenyewe. Ndiyo maana tunaambiwa
wazi, “Roho ndiyo itiayo uzima (Yn.6:63).
YOTE YAWEZEKANA KWAKE AAMINIYE [MK.9:23], WALA HALITAKUWAKO NENO LISILO WEZEKANA KWENU [MT.17:20]
Tumekwisha kupata tafsiri ya neno “IMANI” kwamba ni kuwa na hakika ya
mambo yatarajiwayo; ni bayana ya mambo yasiyoonekana. Au, kwa Kiswahili
kinachosemekana kwamba ni cha kisasa, “Imani ni kuwa na hakika ya mambo
tunayotumainia; ni kusadiki kabisa mambo tusiyoyaona. Imani ni
kuyachukulia tusiyoyaona, kwamba yamekwisha kutimilika 100%.
IMANI KATIKA NINI? AU KUAMINI NINI?
Baada ya kujua maana ya neno imani, swali linalofuata ni “KUAMINI
NINI?” Vinginevyo tutabaki hewani, na hapo ibilisi atakuwa amepewa
nafasi.
Katika hili, Bwana Yesu anajibu, “Mwaminini Mungu”
(Mk.11:22), ambaye kwake yote yawezekana (Mk.10:27) mpate kuuvaa
utimilifu wote wa uwezo wa Mungu wa kuhamisha hata milima (Mk.11:23).
KUMWAMINI KRISTO NENO LA MUNGU
Katika Yn.14:1 KRISTO NENO LA MUNGU atuambia, “Mnamwamini Mungu,
niaminini na Mimi”. Kristo Neno la Mungu alikwisha kutudhihirishia
kwamba Baba yake aliyemtuma ni kweli (Yn.8:26). Jambo hili lilikwisha
kushuhudiwa na Yeye ashuhudiaye, Roho Mtakatifu (1 Yoh.5:7) kwamba Mungu
ni kweli (Yn.3:33).
Sasa hapa atuambia, “Mnamwamini Mungu aliye
kweli; niaminini na Mimi niliye Neno lake. Yn.17:17 anatusisitizia
kwamba Mungu aliye kweli na Neno lake ni Umoja, pale alipomwambia Baba,
“Uwatakase kwa ile kweli; Neno lako ni kweli.
MANENO YA YESU MWISHONI MWA MAISHA YAKE DUNIANI
Bwana Yesu akawaambia wanafunzi wake “Hata bado ningali ninayo mengi ya
kuwaambia lakini hamwezi kuyastahimili hivi sasa. Lakini yeye
atakapokuja huyo Roho wa kweli, atawaongoza awatie kwenye kweli yote…….”
(Yn. 16:12-13)
Baada ya kufufuka kwake, pamoja na mengineyo,
aliwaambia, “Amani iwe kwenu; kama Baba alivyonituma mimi, mimi nami
nawatuma ninyi. Naye akiisha kusema hayo, AKAWAVUVIA, AKAWAAMBIA,
POKEENI ROHO MTAKATIFU”. ( Yn.20:21-22)
Hapo ndipo utume wa
mitume ulipotimilika. Maana, pamoja na kuwatuma, amewatia Roho
Mtakatifu wa kuwaongoza awatie kwenye kweli yote. Na ndiyo maana Paulo
ana ujasiri wa kusema “Lakini ijapokuwa sisi au malaika wa mbiguni
atawahubiria ninyi Injili yoyote isipokuwa hiyo tuliyowahubiria na
alaaniwe (Gal.1:8-9). Hata anatushangaa pale tunapowavumilia wale
wanaohubiri mayesu wengine na hata kupokea maroho mengine (2Kor.11:4).
Kwa nini Paulo Mtume asema haya yote? Ni kwa sababu wao walimpokea
Roho Mtakatifu halisi (Original) kutoka kwa Kristo Neno la Mungu
mwenyewe. Roho waliyempokea kutoka kwa Yesu asingeweza kuwa roho ya
upotevu.
Wakiwa wanaongozwa na Roho wa Kweli, kwenye kweli yote wanatufundisha yafuatavyo:
(1) Basi nasema nendeni kwa Roho, wala hamtazitimiza kamwe tamaa za
mwili, kwa sababu mwili hutamani ukishindana na Roho na Roho kushindana
na mwili; kwa maana hizi zimepingana HATA HAMWEZI KUFANYA MNAYOTAKA
(Gal.5:16-17).
(2) Mmetengwa na Kristo ninyi mtakao kuhesabiwa
haki kwa sheria; mmeanguka na kutoka katika hali ya neema. Maana sisi
kwa Roho tunalitazamia tumaini la haki kwa njia ya imani (Gal.5:4-5).
(3) “….wakapate utajiri wote wa kufahamu kwa hakika wapate kujua kabisa
siri ya Mungu, yaani Kristo; ambaye ndani yake Yeye hazina zote za
hekima na maarifa zimesitirika (Kol.2:2-3).
(4) “Angalieni mtu
asiwafanye mateka kwa elimu yake ya bure na madanganyo matupu kwa jinsi
ya mapokeo ya wanadamu; kwa jinsi ya mafundisho ya awali ya ulimwengu
wala si kwa jinsi ya Kristo. Maana katika Yeye unakaa utimilifu wote wa
Mungu, kwa jinsi ya kimwili. Na ninyi mmetimilika katika Yeye aliye
kichwa cha kila enzi na mamlaka Kol.2:8-10.
(5) Kwa kuwa katika
Yeye ilipendeza utimilifu wote ukae; na kwa Yeye kuvipatanisha vitu
vyote na Nafsi yake akiisha kufanya amani kwa Damu ya Msalaba wake
(Kol.1:19-20a).
(6) Watu wote wamefanya dhambi na kupungukiwa na
utukufu wa Mungu; wanahesabiwa haki bure kwa neema yake, kwa njia ya
ukombozi ulio katika Kristo Yesu; ambaye Mungu amekwisha kumweka awe
upatanisho kwa njia ya imani katika Damu yake. apate kuonesha haki yake,
kwa sababu ya kuziachilia katika ustahimilifu wa Mungu dhambi zote
zilizotangulia kufanywa (Rum.3:23-25).
(7) Kristo akajitoa ili makusudi alitakase na kulisafisha Kanisa lake kwa maji katika Neno…..” Efe.5:26-27
(8) Hivyo, ilimpasa kufananishwa na ndugu zake katika mambo yote, apate
kuwa kuhani mkuu mwenye rehema, mwaminifu katika mambo ya Mungu, ili
afanye kafara ya suluhu kwa dhambi ya watu wake (Ebr.2:17).
(9)
Ndipo aliposema, “Tazama, nimekuja niyafanye mapenzi yako. Aondoa la
kwanza kusudi alisimamishe la pili; katika mapenzi hayo, mmepata utakaso
kwa kutolewa Mwili wa Yesu (Neno la Mungu) mara moja tu. (Ebr.10:7-10)
Na kila kuhani husimama kila siku akifanya ibada, na kutoa dhabihu zile
zile mara nyingi ambazo haziwezi kabisa kuondoa dhambi. Lakini huyu
alipokwisha kutoa kwa ajili ya dhambi dhabihu moja idumuyo hata milele
aliketi mkono wa kulia wa Mungu. Maana kwa toleo moja amewakamilisha
hata milele hao wanaotakaswa. Ndipo asemapo, “Dhambi zao na uasi wao
sitaukumbuka tena kabisa. Basi ondoleo la hayo likiwapo, hapana toleo
tena kwa ajili ya dhambi (Ebr.10:11-18).
(10) Katika Ebr.10:19-23
tunaambiwa, “Basi, Ndugu kwa kuwa tuna ujasiri wa kupaingia patakatifu
kwa Damu ya Yesu, njia ile aliyotuanzia iliyo mpya, iliyo hai, ipitayo
katika pazia yaani Mwili wake; na kuwa na Kuhani Mkuu juu ya Nyumba ya
Mungu; NA TUKARIBIE WENYE MOYO WA KWELI KWA UTIMILIFU WA IMANI HALI
TUMENYUNYIZIWA MIOYO TUACHE DHAMIRI MBAYA, TUMEOSHWA MIILI KWA MAJI
SAFI. NA MLISHIKE SANA UNGAMO LA TUMAINI LETU LISIGEUKE; MAANA YEYE
ALIYEAHIDI NI MWAMINIFU”.
(11) Wala hawezi kujikana mwenyewe ‘
kama sisi hatuamini, yeye hudumu wa kuaminiwa. Kwa maana hawezi kujikana
mwenyewe”. (2Tim.2:13).
Hayo ndiyo wanayotufundisha Mitume wa Yesu Neno la Mungu kuhusu swala la ondoleo la dhambi.
YESU MWENYEWE ANASEMAJE KUHUSU ONDOLEO LA DHAMBI
Katika Mt.20:28 atuambia, “Kama vile mwana wa Adamu asivyokuja
kutumikiwa, bali kutumika, na kutoa Nafsi yake iwe fidia ya wengi”. Na
katika Mt.26:28 anaweka wazi zaidi: “Kwa maana hii ndiyo Damu yangu ya
agano jipya imwagikayo kwa ajili ya wengi kwa ondoleo la dhambi”.
MATOKEO YA UTAKASO AU ONDOLEO LA DHAMBI
Kwa kadiri ya Ebr.10:14, tokeo la utakaso ni kukamilishwa hata milele.
Ukamilishwaji huu upo katika kushirikishwa Roho Mtakatifu (1Yoh.4:13);
tendo ambalo hufanyika kwa kunyweshwa Roho mmoja (1Kor.12:13) na kumvaa
Kristo Neno la Mungu (Gal.3:27); na hivyo kuwa mwana wa Mungu (Gal.3:26)
kuwa kama Mungu mwenyewe alivyo (1Yoh.4:17). Na hivyo, kushiriki tabia
ya Uungu (2Pet.1:4) ikiwa ni pamoja na uwezo.
Ili kufikia hilo,
siri ya Mungu iko katika Yesu Neno la Mungu, nayo ni kuamini utakaso kwa
Damu ya Yesu ambaye ni Roho Mtakatifu ambaye ndani yake mna maji hai
(Yn.4:10, 14; 7:37-39); naye huyu Roho yumo ndani ya Neno kama vile Neno
alivyo ndani ya Roho na Kweli, katika Utatu wao Mtakatifu.
HITIMISHO
Imani ni kuwa na hakika ya mambo yatarajiwayo, ni bayana ya mambo
yasiyoonekana. Tena imani ni nguvu kuu; kwani yote yawezekana kwake
aaminiye, wala hakuna Neno lisilowezekana kwake aaminiye. (Mk.9:23;
Mt.17:20)
Lakini nguvu hiyo iko katika kushirikishwa utimilifu
wote wa Mungu (Efe.3:19) kwa kunyweshwa Roho Mtakatifu (1Kor.12:13;
1Yoh.4:13), na hivyo kumvaa Kristo Neno la Mungu (Gal.3:27).
Ili
kunyweshwa Roho Mtakatifu, kuzaliwa mara ya pili (Yn.3:3, 5), sharti mtu
awe amepokea upatanisho na utakaso kwa njia ya imani katika Damu ya
Yesu (Rumi.3:25; Kol.1:20; Ebr.10:19-22) iliyomo katika Neno la Mungu
(Efe.5:26-27).
Nje ya hayo tunaambiwa “MAANA TUKIFANYA DHAMBI
KUSUDI BAADA YA KUUPOKEA UJUZI WA ILE KWELI, HAIBAKI TENA DHABIHU KWA
AJILI YA DHAMBI; BALI KUNA KUITAZAMIA HUKUMU YENYE (KWENYE) KUTISHA NA
UKALI WA MOTO ULIO TAYARI KUWALA WAO WAPINGAO. MTU ALIYEIDHARAU SHERIA
YA MUSA HUFA PASIPO HURUMA KWA NENO LA MASHAHIDI WAWILI AU WATATU.
MWAONAJE? HAIKUMPASA ADHABU ILIYO KUBWA ZAIDI MTU YULE ALIYEMKANYAGA
MWANA WA MUNGU NA KUIHESABU DAMU YA AGANO ALIYOTAKASWA KWAYO KUWA NI
KITU OVYO, NA KUMFANYIA JEURI ROHO WA NEEMA? (EBR.10:26-29).
Kwa
maana asema, “Kwa wakati uliokubalika nilikusikia. Na katika siku ya
wokovu nilikusaidia, tazama, wakati uliokubalika ndio sasa, tazama, siku
ya wokovu ndiyo sasa (2Kor.6:2).
Chakuzingatiwa kwa makini ni
ukweli huu kwamba kumwamini Mungu kama Mungu hakuna thawabu yoyote.
Tendo hilo hata mashetani hulifanya; tena kwa kutetemeka.( Yak.2:19).
Bali tunalotakiwa sisi ni kulitambua na kuliamini lile tendo timilifu
la kutohesabiwa makosa ( Rumi.8:33-34, 2Kor.5:19) na kutakaswa kwa maji
safi yaliyomo katika damu ya Kristo Neno la Mungu ambaye ni Roho
Mtakatifu ( Efe 5:25-27, Ebr.10:19-22, Yoh.7:37-39)
Katika yote,
siachi kumshukuru Mungu wa pekee wa kweli kwa udhihirisho wake kwenye
Mtaguso wa Vatikani II na katika Mababa (Mapapa) Mtakatifu waliofuata
katika utayari wao kutekeleza kusudio lake la kuumba upya dunia yake
inayoharibiwa na Yule mwovu.
Kwa namna ya pekee nazingatia zile
kauli za ule Waraka wa Kichungaji “UT UNUM SINT” ulioandikwa na Mt. Papa
Yohani Paulo II ambao kwao ametutaka tuwe waaminifu kwa Injili,
kuiongokea Injili kwa kina, kuwa na fikra mpya na matazamo mpya wa mambo
(Kifungu Na.15). Katika Waraka huo pia Baba ametuhimiza kuiheshimu
Kweli zaidi ya chochote kile, kwa hoja kwamba Kweli ni Mungu (Kifungu
18) na kwamba kwa hoja hiyo hiyo, namna zetu za kuielezea imani yetu
zisiwe kuzuizi katika mchakato wetu wa kutafuta Kweli (Kifungu Na:36).
Na tubarikiwe sote sawasawa na Efe.1:3.
LUKA ROKI MAGHALI CHAMAYOMBE
0787 765 759
0714 118 428
0753 298 707
Chamayombe37@gmail.com
Subscribe to:
Post Comments (Atom)



0 comments:
Post a Comment