Subscribe:

Sample text

Sample Text

Wednesday, 4 October 2017

KANISA LA YESU [NENO LA MUNGU

1. Kanisa la Yesu ni moja Takatifu, Katoliki na la kimitume. Kwamba Kanisa la Yesu ni moja ni kwa sababu, kwa njia ya Kristo, pamoja naye na ndani yake, kila mdau wa Kanisa la Yesu yuko ndani ya kila Nafsi ya umoja wa Nafsi Tatu za Mungu; na kila Nafsi ya Utatu Mtakatifu yuko ndani ya kila mdau wa Kanisa la Yesu. Na kwa utaratibu huo ni kwamba kila mdau wa Kanisa la Yesu yuko ndani ya kila mdau wa Kanisa la Yesu (Yn.17:21-23). Kwa jinsi hii wadau wa Kanisa la Yesu, kwa pamoja huwa maskani moja ya Mungu pekee wa kweli katika Roho (Efe.2:18-22)
2. Kanisa la Yesu ni Takatifu kwa sababu hutakaswa sawasawa na maombezi ya Yesu (Yn.17:17, 19), na kwa Neno la Mungu kweli (Efe.5:25-27); Ebr.10:1923). Na kwa utakaso huo hukamilishwa katika Umungu huo kwa kunyweshwa Roho wa kweli (1Kor.12:13). Na hivyo kumvaa Kristo kushiriki utimilifu wa Mungu. Katika hali hiyo, hatendi tena dhambi (Yoh.3:6, 9; 5:18).
3. Kanisa la Yesu ni Katoliki. Neno Katoliki” maana yake halina mipaka (Universal).
Sasa Kanisa la Yesu ni Katoliki kwa sababu kwanza Yesu alionja mauti kwa ajili ya kila mtu (Ebr.2:9); ili kujikusanyia watu wake waliotawanyika wawe wamoja tena (Yn.11:52), chini ya Mchungaji Mmoja (Yn.10:16); kuwanywesha Roho mmoja ili wawe mwili mmoja (1Kor.12:13); na hivyo kumvaa Yesu bila ubaguzi wowote (Gal.3:27). Ili kuwa Roho moja na Yesu (1Kor.6:17) na hivyo kuwa mdau wa Kanisa na Yesu (Gal.3:29; Rum.8:9) popote pale walipo.
4. KANISA LA YESU ni LA KIMITUME
Kwa kadiri ya Yn..11:52, Kanisa la Yesu ni kusanyiko la watoto wa Mungu waliotawanyika ili wawe wamoja tena. Mitume walikuwa wa kwanza kuchaguliwa wawe Kanisa moja la Yesu. Kwa muda wa miaka mitatu wakaandaliwa jinsi ya kuwa wadau wa Kanisa la Yesu.
Ili kuwa mdau wa Kanisa la Yesu sharti mtu awe Roho moja na Yesu (1Kor.6:17) kwa kunyweshwa Roho wa kweli (1Kor.1Kor.12:23) ili hivi kwamba mtu kuwa ndani ya Mungu na Mungu ndani ya mtu, kuwa umoja na Mungu (1Yn.4:13). Hivyo ndivyo mtu huwa wa Yesu kweli (Gal.3:29; Rumi 8:9).
Katika hali hiyo mtu amekuwa amezaliwa mara ya pili katika Umungu pekee wa kweli (Yn.3:3, 5; Gal.3:26). Ili hili lipate kutendeka, sharti mtu apokee, ile neema au zawadi ya upatanisho kwa njia ya imani katika Damu ya Yesu; (Rumi 3:24—26; Ebr.10:19-23). Kwani haitawezekana Mungu kurudi ndani ya mtu kabla ya Upatanisho.
Kwa kupokea upatanisho kwa njia ya imani katika Damu ya Yesu, Mungu Baba huziachilia katika ustahimili wake dhambi zote zilizotangulia kufanywa (Rum.3:25); na kumhesabia mtu husika haki katika Kristo Yesu (2Kor.5:21).
Pamoja na Yesu kuwafundisha mitume wake mengi kuhusu Ufalme wa mbinguni, lakini katika Yn.16:12-15. Bwana Yesu awaambia mitume wake “Hata bado ningali ninayo mengi ya kuwaambia lakini, hamwezi kuyastahimili hivi sasa. Lakini Yeye atakapokuja, huyo Roho wa kweli, atawaongoza awatie kwenye kweli yote ….”. Kujua mambo ya Mungu, sharti mtu awe na Roho wa Mungu. Na Roho wa Mungu hupatikana baada ya Yesu kutukuzwa (Yn.7:39)
Hii inatukumbusha kile Yesu alichokisema kuhusu mito ya maji yaliyo hai ambayo hutoka ndani yake yeye aaminiye. Wakati huo Roho huyo alikuwa hajaja kwa sababu Yesu alikuwa hajatukuzwa (Yn.7:37-39).
Hii inamaanisha kwamba lile swala kuu la jinsi ya ujio wa Roho wa kweli na jinsi ya uendeshaji wa Kanisa lake na mengineyo mengi, Yesu hakuwaambia Mitume wake kwa sababu ni maswala yanayotendwa na Roho wa kweli mwenyewe akiwa ndani yake mtu husika; kama anavyo-tuambia katika 1Kor.2:12, “Lakini sisi hatukupokea roho ya dunia, bali Roho atokaye kwa Mungu, makusudi tupate kuyajua tuliyokirimiwa na Mungu: (Soma 1Kor.2:10-16).
Mitume walimpokea Roho wa kweli pale walipovuviwa na Yesu na kuambiwa pokeeni Roho Mtakatifu (Yn.20:22). Tangu hapo Bwana Yesu kwa huyo Roho wake wa kweli akakamilisha ngwe nzito iliyobaki ambayo sisi sasa twaipata katika nyaraka zao hawa mitume, huyo Roho wa kweli na jinsi ya kumpata.
Kwa sababu hiyo, kupuuza Nyaraka za Mitume ni janga kubwa mno ambalo mtu huweza kujiingiza kwa hasara yake mwenyewe na hata wale anaowaongoza, ikiwa mtu huyo ni Kiongozi. Kweli yote kuhusu elimu ya ufalme wa mbinguni hupatikana katika Nyaraka za Mitume. Kuhubiri habari za Yesu nje ya mahubiri ya Mitume ni laana (Gal.1:8-9) kwa sababu hayo yatakuwa ni mahubiri yalio nje ya kweli yote. Yn.16:12-13) aliyotuletea Bwana Yesu.
Kwa kufanya dhambi ya kuwapuuza Mitume wa Yesu, badala ya kuhubiri taratibu za kuondokana na utumwa wa dhambi, Makanisa huishia kuhubiri mungu pesa kwa masilahi ya wahusika. Badala ya kumhubiri Mungu wa Mbinguni, makanisa humhubiri mungu wa kuzimu kwa maangamizi ya wahubiri na wahubiriwa, wenyewe bila kujua. Ni HATARI!
5. KANISA LA YESU NI LA ULIMWENGU WA MBINGUNI
Pamoja na sifa nne hapo juu, kutokana na ile simulizi ya Tajiri na Lazaro (Lk.16:19-31), na kujifunua kwa Bwana Yesu, Neno la Mungu, kwamba Yesu ni wa juu, si wa Ulimwengu huu (Yn.8:23) tunajifunza kwamba mtu hukabiliwa na aina mbili za ulimwengu; yaani ulimwengu wa Mungu wa mbinguni na ulimwengu wa kuzimu, kule yule mwasi alikoshushwa kutokana na dhambi yake ya kujikweza (Isa 14:13-15).
Katika kutuombea kwa Baba, Bwana Yesu alimwambia Baba “Neno lako nimewapa na ulimwengu umewachukia kwa sababu wao si wa ulimwengu kama mimi nisivyo wa ulimwengu. Mimi siombi kwamba uwatoe ulimwenguni; bali uwalinde na Yule mwovu; maana wao si wa ulimwengu kama mimi nivyo wa ulimwengu (Yn.17:14-16). Tena asema, Baba hao ulionipa nataka wawe pamoja nami popote nilipo (Yn.17:24).
Tena tunasoma, Akatufufua pamoja naye, akatukatisha pamoja naye katika ulimwengu wa Roho katika Kristo Yesu (Efe.2:6). Ni akina nani hao? Hao ndio Kanisa la Yesu aliojitakasia kwa maji katika neno; apate kujiletea Kanisa tukufu lisilo na dosari wala kunyanzi, wala lolote kama hayo; bali liwe takatifu lisilo na mawaa (Efe.5:25-27).
Kwa njia ya Yesu Kristo, wadau wa Kanisa la Yesu hupata njia ya kumkaribia Baba katika kunyweshwa Roho mmoja(Efe.2:18; 1Kor.12:13). Na katika Kristo Yesu wadau wa Kanisa lake wamejengwa pamoja kuwa maskani ya Mungu katika Roho (Efe.2:22).
Kwa mantiki hii wadau wa Kanisa la Yesu wanapaswa kwenda kwa Roho (Gal.5:16-17). Kwa kadiri ya Kol.3:1-3) wanapaswa kutafuta yaliyo juu Kristo aliko; Kwani Uhai wao umefichwa pamoja na Kristo katika Mungu (Kol.3:1-3). Uenyeji wao uko mbinguni (Fil.3:20). Katika umoja wa nafsi Tatu, kweli na Neno na Roho wa Kweli (1 Yon.5:7 au 8). Wao ni washirika wa tabia ya Mungu wa mbinguni (2 Pet.1:3-4). Hapa duniani wadau wa Kanisala Yesu wao ni wageni (1Pet.1:17). Hawapaswi kuipenda dunia (1Yoh.2:15-17). Nao hutambulikana kwa tunda la Roho (Gal.5:22-23).
Kwa kuwa Kanisa la Yesu liko katika ulimwengu wa Mungu aliye Roho, Kanisa hili liko nje ya ile milango 5 ya fahamu za mwili wa nyama; macho, masikio, pua, ulimi na ngozi. Kanisa la Yesu huenda katika Roho na Kweli kwa njia ya imani; kwa maana halisi ya neno hili IMANI, yaani kuwa na hakika ya mambo yatarajiwayo, ni bayana ya mambo yasiyoonekana (Eb.11:1).
Kama tulivyoagizwa katika Gal.5:16-17 kwenda kwa Roho sifa hii ya Kanisa la Yesu inahusu pia zile sifa nne za kwanza za Kanisa la Yesu, kwamba Kanisa la Yesu ni moja Takatifu, Katoliki na la kimitume. Sifa zote zinapata hadhi katika Mungu pekee wa Kweli ambaye ni Umoja wa Nafsi Tatu, Kweli na Neno na Roho wa Kweli (1Yoh.507) 8).
Mungu aliye Roho (Yn.4:24), mwenye Nafsi Tatu, Kweli na Neno na Roho wa Kweli, amejiumbia mtu wake kwa mfano na sura yake mwenyewe (Mw.1:26) na kumshirikisha uzima = Roho wake (Mw.2:7) ili kukidhi mapenzi yake ya kuabudiwa katika Roho na Kweli (Yn.4:23).
Na hilo ndilo Kanisa lake la Ulimwengu wa Mbingun, ambalo ingawa lipo katika ulimwengu huu, lakini halienendi kwa kuangalia vinavyoonekana (2Kor.4:18). Ni Kanisa linaokwenda kwa imani, si kwa kuona (2Kor.5:7). Na Mungu mwenyewe anasema, “Mwenye haki wangu ataishi kwa imani, naye akisitasita, Roho yangu haina furaha naye (Ebr.10:28). Kanisa la Yesu ni la ulimwengu wa mbinguni, ulimwengu wa ROHO.
6. HITIMISHO
Basi kutokana na hayo, mimi binafsi naamini kwamba ule Waraka wa Kichungaji wa Papa Yohani Paulo II, “The Call for Christian Unity (ut unum sint) chini ya uongozi wa Vatikani II, ni uamsho wa kutuamsha sisi sote tuamke na kuondokana kabisa na huu usingizi wa mauti ya milele unaotukabili.
Waraka hututaka kuwa waaminifu kwa Injili. Pamoja na mengineyo mengi tunayoagizwa na Injili, Injili hututaka kwenda kwa Roho wala hatutazitimiza tamaa za mwili ambazo zimeorodheshwa katika Gal.5:19-21, na ambazo wazitendao hawataurithi ufalme wa Mungu.
Kwamba dhambi au maasi hushamiri duniani, kama ilivyoshuhudiwa kwenye Kongamano la Miaka 35 ya Karismatiki Katoliki kule Dodoma, ni kidhibiti tosha kwamba dunia na dini zake huendeshwa kimwili badala ya kwenda kwa Roho kama tulivyoagizwa na Injili. Dunia na dini zake zinaiasi Injili.
Tena, kwa mujibu wa mada ya kuzipima roho; ni dhahiri kwamba Roho wa Kweli amepotezwa. Dunia na dini zake huenenda na roho ya upotevu inayowafanya watu wa Mungu wampoteze Mungu wao wa kweli. Huenenda na Roho ya upotevu inayowafanya watu wa Mungu wampoteze Yesu, Neno la Mungu kweli, na kuenenda na mayesu wengine wa kuzimu.
Sasa wakati umefika wa kudhamiria kwa dhati ya 100% kwenda kwa Roho kama tulivyoagizwa na Injili ya Mitume (Gal.5:16-17; 1:8-9).
Wakati wa kutimilika kwa mapenzi ya Mungu (1Tim.2:4) kwamba watu wote waokolewe (Kol.1:13) na kupata kujua yaliyo kweli (Yn.17:3) sasa umefika.
Wakati umefika sasa wa kuachana kabisa na fikira za kidini ambazo huwapelekesha watu wa Mungu kwa makristo wa uongo (Mk.13:21-22); fikira za kidini ambazo huwapelekesha watu wa Mungu waenende na mayesu wengine au roho nyingine ambazo huwapelekesha watu wa Mungu mbali kabisa na Yesu, Neno la Mungu Kweli (2Kor.11:4; Yn.8:26; 3:33).
Wakati umefika sasa wa kumwambia Yule mungu wa ulimwengu wa kimwili ambaye ni mwuaji, mwongo na baba wa uongo, wakati umefika sisi dunia tumwambie kwa ujasiri 100% maadamu tuna Roho wa Kweli, tumwambie, Umetuonea kwa kutugharagaza katika maasi na maovu yako kiasi cha kutosha. Sasa tunasema BASI!!!” Tumwambie kwa ujasiri yeye na wafuasi wake, wakome na wabaki peke yao huko kuzimu, pande za mwisho za shimo walikoshushwa (Isa.141:15).
Wakati uliokubalika ndio sasa; na siku ya wokovu ambayo Mungu Kweli huwatakia watu wake ndio sasa; na ndio sasa ambapo ataka watu wake kujua Kweli.
Ndugu yangu nikupendaye kwa upendo wa Kristo, fahamu kwamba Nuru ya Yesu imeng’aa gizani wala giza haikuweza (Yn.1:5). Jipe moyo, Yesu ametushindia (Yn.16:33). Na ubarikiwe kwa Baraka zote za kiroho katika Ulimwengu wa Roho ndani yake Kristo, Neno la Mungu Kweli (Efe.1:3), sasa hata na milele!!.....
LUKA ROKI MAGHALI CHAMAYOMBE
0714 118 428
0787 765 759
0753 298 707
Email: chamayombe37@gmail.com

0 comments:

Post a Comment